KATIKA
mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga, uliofanyika katikati ya
wiki ulileta furaha na huzuni kwa upande mmoja. Kuna waliofurahia na wale
waliolala mapema sikuhiyo.
Mchezo
huo ambao unaashiria kuanza kwa Ligi Kuu, ulizikutanisha timu hizo ambapo Simba
ilifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika
mabao hayo, moja lilifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ huku jingine likiwekwa
kimiani na Felix Sunzu Jr, ambaye pia ndiye aliyetengeneza bao lililopachikwa
na Boban.
Kwa
sasa amekuwa jina kubwa na limekaa mno midomoni mwa washabiki wa Simba, ambao
wanaona ni suluhisho la timu hiyo katika safu ya ushambuliaji.
Kumbuka
mchezaji huyu wa zamani wa Konkola Blades ya Zambia na anayeichezea pia timu ya
taifa ya nchi hiyo, Chipolopolo, aliachwa na Al Hilal inyonolewa na Srojdevic
Milutin ‘Micho’ ikiwa ni miezi sita tu toka atwaliwe na timu hiyo.
Al
Hilal waliamua kuvunja mkataba na Sunzu, baada ya mshambuliaji huyo kudaiwa
kuonyesha kiwango kibovu na kuzidiwa ujanja na Mzimbabwe Sadomba, aliyeonekana
kufumania mno nyavu.
“Ni
kweli, Al Hilal imeamua kusitisha mkataba wake na Sunzu, baada ya kuvunjwa moyo
na kiwango duni alichoonyesha na kocha ameamua kutomchukua kabisa,” ilisema
taarifa ya klabu hiyo.
Sunzu
Jr alionwa na Micho, baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika michuano ya
Kombe la Chalenji mwaka jana, ambapo alikuwa akiichezea Zambia .
Kwa
muda Sunzu, anaonekana kama anayehangaika barabarani na kushindwa kutulia katika
timu moja kwani baada ya kuwemo katika kikosi cha Zambia 2008, alichukuliwa na
Al Masry ya Tunisia , ambako
nako alitemwa kwa sababu kama hizo.
Aliporudi
Zambia , aliamua kujiunga na
timu ya nyumbani kwao ya Konkola Blades, lakini akaondoka na kwenda kujiunga na
Lupopo ya Lubumbashi ,
mwaka 2010 na yaliposhindikana alirejea tena Konkola Blades kwa mara ya tatu.
Katika
michuano ya Kombe la Chalenji, Sunzu akaonyesha kiwango kikubwa na kufanikiwa
kufunga mabao matano, hivyo kuivutia Al Hilal iliyoamua kumchukua.
Sunzu
akajumuishwa katika ziara ya timu hiyo huko Misri na Israel kabla ya
kuchukuliwa na Al Hilal, huku kukiwa na madai TP Mazembe nayo inamtaka, timu
ambayo anachezea pia ndugu yake, Stopilla.
Baada
ya Al Hilal kumtema, Simba ikaingia kati na kuanzia kumfuatilia mshambuliaji
huyo na awali timu hiyo ilionekana kutaka kuiingiza Simba ‘king’ kwa madai bado
haijamtema ili ipate fedha.
Sunzu,
anaonekana ni mkali akiwa zaidi na Wazambia wenzake kwani alikuwa ndiye
mfungaji bora wa michuano ya Chalenji 2010.
Wakati
huo Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geodfrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wako katika
mazungumzo ya kina ya kuhakikisha wanamtwaa mshambuliaji huyo.
“Ni
mmoja kati ya wachezaji wazuri zaidi na naamini akifika hapa atatusaidia kwa
kiwango kikubwa, kwani ana uwezo mkubwa ambao utaisaidia zaidi Simba,” alisema
Kaburu wakati huo.
Kwa
sasa imeonekana kweli, kwani Sunzu ameondokea kuwa mshambuliaji tumaini ndani
ya Simba na anayeweza kuisaidia zaidi katika Ligi Kuu iliyoanza jana.
Ni nani?
Felix
Mumba Sunzu alizaliwa Mei 2, 1989 katika mji wa Chingola nchini Zambia, ambaye
kwa sasa anaichezea Simba.
Sunzu
alianza maisha ya soka kwa kuichezea Afrisport F.C na mwaka 2005 alijiunga na
timu aliyoichezea baba yake ya Konkola Blades, lakini baada ya mwaka mmoja wa
kuichezea timu ya vijana mwaka 2007 akapandishwa hadi timu ya wakubwa.
Katika
msimu wake wa kwanza aliichezea Konkola Blades mechi 25 na kufunga mabao 15,
lakini Februari 2007 akachukuliwa kwa mkopo na timu ya AS Marsa, ambapo
alicheza mechi 16 na kufunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya Tunisia.
Lakini
Juni 2008 akarudi Konkola Blades lakini Septemba 2, 2008 akapelekwa kwa mkopo
katika timu ya LB Chateauroux inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Ufaransa kwa
muda wa mwaka mmoja.
Julai
2009 akarudi AS Marsa ambaye alicheza Oktoba 29, kabla ya timu hiyo kuamua
kuachana naye, ambapo akiwa hapo alicheza mechi mbili tu.
Alishawahi
kukaririwa akisema, kwa sasa amekuja nchini kuhakikisha anarejesha heshima yake
na kuwataka mashabiki wa Simba, wasubiri vitu vingi zaidi kutoka kwake.
Tutake
tusitake, Sunzu anaonekana kurudi katika makali, kwani katika mchezo dhidi ya
Yanga, alitumia uzoefu wake kuifanya beki ya timu hiyo ionekane imepwaya.
Ingawa
ni mchezo mmoja tu, Sunzu anatakiwa kuonyesha vitu zaidi ili mashabiki wa Simba
waendelee kumuamini, kwani kinyume chake anaweza kujikuta akizidi kutangatanga.
WASIFU
JINA:
Felix Mumba Sunzu
KUZALIWA:
Mei 2, 1989
ALIPOZALIWA:
Chingola, Zambia
UREFU:
Futi 5 inchi 8
NAFASI:
Mshambuliaji
TIMU:
Simba
JEZI
Na: 10
Timu
za Vijana
2002-2005
Afrisport F.C
2005-2007
Konkola Blades
Timu
za Wakubwa
2007-
Konkola Blades
2007-2008
AS Marsa (mkopo)
2008-2009
LB Châteauroux (mkopo)
2009
AS Marsa (mkopo)
Timu
ya Taifa
2005-2007
Zambia U-21
2008-
Zambia
0 comments:
Post a Comment