MSHAMBULIAJI wa Simba Emmanuel Arnold Okwi, pamoja na
uhodari mkubwa alionao amejikuta akiingia kwenye matatizo mara kwa mara katika
klabu hiyo.
Okwi aliisaidia timu yake ya taifa ya Uganda The Cranes
kutwaa ubingwa wa Kombe CEFACA Tusker Challenge, na alikuwa ni mmoja wa
wafungaji bora.
Pia katika timu yake ya Simba mchezaji huyo amekuwa ni
tishio mbali ya kosa kosa nyingi ambazo zimekuwa zikiwakera mashabiki wa timu
hiyo ambao huwa wanaona kama anafanya makusudi.
Mashabiki wengi wa Simba wamekuwa wakikosa imani na mchezaji
huyo, hasa pale timu yake inapocheza na Yanga, ambapo huwa anadaiwa kucheza
chini ya kiwango.
Wakati timu yake ikiwa katika maandalizi ya mchezo wao wa
Kombe la Shirikisho (CAF) na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Okwi ameshindwa kuripoti katika timu yake tangu aondoke Desemba mwaka
jana, kwa madai kwamba anakwenda kula
sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, lakini hadi leo hajawasili nchini.
Pamoja na ukimya huo, uongozi wake ulijaribu kumtafuta kwa
kumpigia simu yake ya mkononi lakini ilikuwa imezimwa, huku zikizagaa taarifa
kwamba mchezaji huyo amekwenda kufanya majaribio Iceland.
Tangu taarifa hizo ziripotiwe, siku nne kabla uongozi wa
Simba ulifanikiwa kumpata baada ya simu yake ya mkononi kuwa hewani, na katika
kujitetea kwake Okwi alidai kwamba alikuwa anaumwa.
Tangu atoe taarifa hizo inakwenda wiki ya pili sasa Okwi
hapatikani tena kwenye simu yake ya mkononi, hali ambayo imewafanya viongozi
wake waingiwe na hofu.
Vituko hivyo vya Okwi vinazidi kuwapandisha hasira
wana-Simba ambao huwa wanaamini kwamba mchezaji huyo huwa anatumiwa na watani
zao Yanga.
Tukio ambalo litakuja kukumbukwa ni lile la Oktoba 29 mwaka
jana, katika mchezo wa Ligi Kuu, baada ya mchezaji huyo kukosa kosa mabao mengi
mara baada ya mchezo kumalizika akajikuta akiingia mikononi mwa mchezaji
mwenzake, kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alikasirishwa na hivyo kumrushia
makonde.
Pamoja na tukio hilo kuonekana wazi, lakini OKwi mwenyewe
alikanusha katika vyombo vya habari, huku akitishia kuvishtaki.
Usumbufu wa Okwi sio Tanzania tu, kwani kuna wakati mchezaji
huyo alikwenda Afrika Kusini kufanya majaribio katika klabu ya Kaizer Chief,
baada ya kufuzu alitakuwa kupimwa afya yake.
Lakini siku ambayo alitakiwa kupimwa mchezaji huyo
hakutokea, na hivyo madaktari kumsubiri kwa zaidi ya masaa matatu bila
mafaniko, hali ambayo ilimfanya wakala wake ajisikie vibaya kwani alioneana
kama na yeye ni taapeli.
Hata alipopatikana mchezaji huyo alidai kwamba alikuwa
amefiwa, hivyo siku ambayo alitakiwa kurudi Afrika Kusini alikosa ndege, na
hivyo akajikuta anakosa ofa hiyo.
Itashangaza kama viongozi wa Simba wataendelea kumfumbia
macho mchezaji huyo ambaye anaonekana ni mtovu wa nidhamu, atazidi kusumbua na
hata wachezaji wenzake watajisikia vibaya kwani wengi wao wanaamini kwamba
baadhi ya viongozi wanamlea sana mchezaji huyo.
Hata hivyo Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema
wamemshitaki mchezaji huyo katika Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo, hivyo akitua
nchini atatakiwa ajisalimishe katika kamati hiyo na kutoa maelezo kabla hatua
nyingine hazijafuatwa.
Okwi alijiunga na
Simba mwaka 2010 akitokea katika klabu ya SC Villa ya Uganda na pia ni mchezaji
wa timu yake ya taifa ya Uganda The Cranes.
Pia mchezaji huyo aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari
akisema kuwa, mkataba wake ukimalizika ndani ya timu hiyo, kama Yanga
watamuhitaji yupo tayari kuichezea, wakati huo Yanga ilikuwa ikinolewa na
Mganda mwenzake, Sam Timbe ambaye alifungashiwa virago na waajiri wake, na
hivyo mikoba yake kurithi Mserbia Kostadin Papic.
WASIFU
WAKE:
JINA:
Emmanuel Arnold Okwi
KUZALIWA:
Desemba 25, 1992
ALIPOZALIWA:
Kampala, Uganda
KLABU
YAKE: Simba SC
KUJIUNGA:
2008
NAFASI:
Mshambuliaji
KLABU
ZA AWALI:
2006-2008:
SC Villa (Uganda)
0 comments:
Post a Comment