DEOGRATIUS Boniventure Munishi ‘Dida’, kipa namba moja wa
Mtibwa Sugar aliyerithi mikoba ya Shaaban Hassan Kado ambaye kwa sasa
anaitumikia klabu yake mpya ya Yanga.
Kutokana na uwezo wake mkubwa akiwa uwanjani timu mbalimbali
zimekuwa zikivutiwa na Dida, hasa Mtibwa Sugar ambao baada ya kumuuza kipa
wake, Shaaban Kado wakaamua kumsajili Dida ili kuziba pengo lake.
Kutokana na umri wake mdogo na umbile lake kubwa, kipa huyu
ambaye amepanda juu, timu nyingi zimekuwa zikimtolea macho, lakini
waliofanikiwa kumpata ni wakata miwa wa Turiani Morogoro Mtibwa Sugar.
Akizungumza na DIMBA hivi karibuni katika mahojiano maalum,
Dida mwenye umri wa miaka 23, alisema kusajiliwa na Mtibwa Sugar msimu huu,
kumemsaidia kuonyesha uwezo wake na pia kunyanyua kipaji chake, kwani anasema
ili uwe mchezaji mzuri ni lazima uwe unacheza mara kwa mara.
“Kitendo cha mchezaji yeyote kukaa benchi muda mrefu bila
kucheza, unaua kipaji chako na pia huwezi kutimiza ndoto zako, kwani ili
mchezaji uuzike katika soko la soka duniani, watu wakuone mara kwa mara
uwanjani.
“Hakuna mchezaji hata mmoja anayependa kusota benchi, lakini
kwa sisi makipa kama sio namba moja unaweza kujikuta ukiishia kusota benchi
msimu mzima,” anasema Dida.
Anasema pamoja na kuwa namba moja katika timu yake ya Mtibwa
Sugar, mara kwa mara amekuwa akiwaachia na wenzake ili wadake, kwani wote wana uwezo
mkubwa, hivyo kitendo cha yeye kukaa kila siku langoni anaweza kuua vipaji vya
wenzake.
Ingawa hakuweka wazi, lakini hapa Dida ni kama anamtumia
ujumbe Juma Kaseja, ili awe anawaachia na wenzake wadake, hasa ikikumbukwa naye
aliondoka Simba kukimbia kuwekwa benchi na mlinda mlango huyo.
Dida aliwahi kudaikia Simba hadi kuwa kipa wa timu ya taifa,
Taifa Stars chini ya Mbrazil, Marcio Maximo na alikuwamo kwenye kikosi
kilichoshiriki michuano ya CHAN Ivory Coast mwaka 2009, kama msaidizi wa
Shaaban Dihile aliyekuwa namba moja.
Alikuwa ana wakati mzuri Simba wakati Kaseja alipokuwa
Yanga, hata hivyo baada ya mwenye namba yake kurejea, alijikuta katika wakati
mgumu hadi akaomba kuachwa na kutimkia Uarabuni, kabla ya kurejea kujiunga na
Mtibwa.
Kihistoria, Dida alizaliwa Aprili 2, mwaka 1989 mjini Dar es
Salaam, na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Madenge iliopo Tandika,
wilayani Temeke, Dar es Salaam na kumaliza mwaka 2000, baada ya hapo akajiunga
na shule ya sekondari ya Makongo ambapo alihitimu mwaka 2004.
“Nilianza kupenda mpira tangu nikiwa nasoma shule ya msingi
na mara kwa mara nilikuwa nachezea timu za mitaani, hata nilipokuwa sekondari
nilikuwa nikichezea timu ya shule,” anasema.
Dida ni mume na baba wa watoto wawili wa kiume, Boniventure
na Luis, anasema aliamua kujikita rasmi kwenye soka mwaka 2006, alipokuwa
akiichezea timu ya Night Star ya Temeke iliyokuwa ikicheza michuano mbalimbali ya
Chama cha Soka Temeke (TEFA).
Baadaye aliihama timu hiyo na kujiunga na Mkunguni FC ya
Ilala mwaka 2007 ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi ya TFF, ambayo kwa bahati mbaya
ilivurunda na kotolewa kwenye ligi hiyo, ingawa yeye alibahatika kusajiliwa na Manyema,
ikiwa Daraja la Kwanza na kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu.
Katikati ya mwaka huo, anasema viongozi wa Simba walivutiwa
naye na hivyo wakamsajili katika timu yao.
“Kwa kweli nilifurahi kusajiliwa na timu kubwa kama Simba,
hivyo nikapanga kuonyesha uwezo wangu ili niwe na mimi napangwa mara kwa mara,”
anasema.
Dida anasema alipokuwa Simba anakiri kwamba alikutana na
makipa ambao walimzidi uwezo, hata hivyo hakujiweka nyuma na hiyo ikawa
changamoto kubwa kwake, makipa aliowakuta ni Kaseja na kipa namba mbili Ally Mustapha
‘Barthez’.
Anasema bahati nzuri alipokuwa Simba alikuwa akidaka baadhi
ya mechi za Ligi Kuu, na kwa mara ya kwanza kucheza michuano ya kimataifa, ni
pale timu yao ilipokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Tusker.
Baada ya kudaka mechi kadhaa katika michuano hiyo, kutokana
na uwezo wake Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo kocha akiwa
Mbrazil Marcio Maximo alivutiwa naye na hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2008,
akaitwa kwenye timu ya taifa.
Kibarua cha kwanza alichokutana nacho ni kwenye timu ya
taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars iliyokuwa ikishiriki michuano ya
Kombe la Challenge mjini Kampala, Uganda.
Anasema mechi ambayo aliidaka ya kwanza ni pale Kili Stars
walipocheza na Rwanda wakafanikiwa kuwafunga 2-0, na ile ya wenyeji Uganda
ambayo walifungwa mabao 2-1 yeye akiwa langoni.
“Kwa kweli nilifarijika sana kwa matokeo hayo, kwani ndio
kwanza niliitwa kwenye timu ya taifa, lakini kutokana na uwezo wangu kocha
Maximo aliniamini na kunipanga mimi,” anasema.
Mwaka 2010 Dida anasema alichukuliwa na Al- Itihad ya
Thuwaiq, Oman baada hya kumaliza mkataba wake Simba.
“Baada ya kumaliza mkataba wangu wa miezi mitano, nikarudi
nchini na kukutana na Mtibwa Sugar ambao walinisajili msimu huu, na mimi
ninawaahidi sitawaangusha,” anasema.
Katika tukio ambalo Dida anasema hata kuja kusahau katika
maisha yake, ni pale alipokuwa Simba ambapo katika mechi moja wapo za Ligi Kuu,
walicheza na Toto African mjini Mwanza na kufungwa mabao 4-2.
“Mimi ndio nilikuwa langoni kwa kweli kipigo kile huwa
sikisahau siku zote katika maisha yangu, kwani tangu kuanza kudaka timu
mbalimbali sikuwahi kufungwa mabao manne, halafu kilichokuwa kikiniuma zaidi ni
kufungwa na timu ndogo kama ile,”anasema.
Akizungumzia Ligi Kuu mzunguko wa pili, Dida anasema ligi ni
ngumu kwani kuna timu ambazo zitakuwa zikipigania zisishuke daraja na nyingine
kutaka kutwaa ubingwa hivyo ushindani utakuwa mkali sana.
“Mimi nawahakikishia mashabiki wa Mtibwa Sugar kwamba
tutajitahidi kuwapa raha na hatutawaangusha kwa kushirikiana na wenzangu, umoja
wao ndio mafanikio yetu,” anasema.
Dida anasema anashukuru Mungu kwamba, timu yao inamashabiki
wengi sana na wamekuwa wakiwapa sapoti kubwa ili kuhakikisha wanafanya vizuri
katika michuano mbalimbali.
Malengo yake ya baadaye ni kucheza soka la kulipwa, muhimu
ni kumuomba Mungu ili aweze kufanikisha malengo yake, kwani anaamini bila
kumtanguliza Mungu kwa kila jambo hakuna mafanikio yoyote.
“Mimi siku zote namuomba Mungu, kwanza anipe uhai zaidi na
kisha kunijalia yale ambayo nayahitaji, siku zote sitachoka kumuomba yeye,”
anasema
WASIFU WAKE:
JINA: Deogratius Boniventure Munishi
KUZALIWA: Aprili 6, 1989 (Miaka 23)
ALIPOZALIWA: Dar es Salaam
KLABU YAKE: Mtibwa Sugar
MWAKA KLABU
2007-2008: Manyema FC
2008-2009: Simba SC
2010-2011: Al- Itihad (Oman)
0 comments:
Post a Comment