Mwape katika mechi na El Merreikh ya Sudan Julai mwaka jana |
Mwape na familia yake |
ALITUA Yanga katika dirisha
dogo la usajili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, lakini kufika
Oktoba mwaka jana zikaanza tetesi kwamba, Davies Robby Mwape anaweza kuachwa
katika dirisha dogo la usajili wa Yanga msimu huu.
Kwa nini? Kuumia mara kwa
mara, kuliwafanya viongozi wa klabu hiyo wahisi mchezaji huyo amefikia ukingoni
kisoka, lakini dakika 90 za mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya watani wa
jadi, Simba zilitosha kumnusuru Mzambia huyo kutupiwa virago Jangwani.
Mwape aliifunga bao pekee la
ushindi Yanga katika dakika ya 72, baada ya kutumia vizuri makosa ya safu ya
ulinzi ya ulinzi ya Simba.
Victor Costa alipiga mpira
ili kuuondosha kwenye hatari, lakini ukamgonga Juma Said Nyosso, ambaye
alizubaa ‘kuuongezea safari’ hadi Mwape akauwahi na Juma Kaseja alipotoka
langoni, akamrahisishia kazi Mzambia huyo kwa kufunga bao hilo.
Mwape alikuwa nje ya Uwanja
wakati Yanga inafungwa 2-0 na mahasimu wao hao katika mechi ya Ngao ya Jamii,
Agosti 17, mwaka jana, kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli, lakini Oktoba
31, mwaka jana alikuwa bora na kudhihirisha umuhimu wake kwenye mechi za watani
wa jadi.
Machi 5, 2011 Mwape alikuwa
anaelekea kufunga bao katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu dhidi ya Simba,
lakini beki Juma Nyosso akamkwatua kwenye eneo la hatari na refa Orden Mbaga
akaamuru ipigwe penalti, iliyokwamishwa kimiani na Stefano Mwasyika dakika ya
59, kabla ya Mussa Hassan Mgosi kuisawazishia Simba dakika ya 73.
Hata hivyo, wakati Yanga ipo
katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, mshambuliaji huyo ameshindwa
kuwasili kujiunga na wenzake.
Nini kinaendelea? Mwape
anasema hayuko fiti kwa asilimia 100, ila haumwi wala si majeruhi. Uongozi wa
Yanga unasema Mwape amebaki kwao anajitibu na amepewa ruhusa na uongozi.
Anajitibu nini ikiwa haumwi?
Ipo siri kubwa ambayo pande zote mbili zinaificha na itakuwa vigumu yeyote
kujua bila ya wahusika kufunguka.
MWAPE NI NANI?
Davies Robby Mwape,
mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Konkola Blades ya Zambia, ambaye kusajiliwa
kwake Yanga kulitokana na kufahamiana kwake na kocha wa Yanga, Kostadin Bozidar
Papic ambaye aliwahi kufanya naye kazi Afrika Kusini.
Lakini ni mwandishi mmoja wa habari
alimuunganisha tena Mwape na Papic baada ya kupotena. “Rafiki yangu mmoja
mwandishi wa habari hapa Tanzania alinitaarifu kama Papic ananitafuta na sasa
yuko Yanga, kwa kuwa Papic alikuwa kocha wangu wakati nacheza Orlando Pirates,
nikakubali, akaniunganisha naye hatimaye mpango ukafanikiwa na nikaja Yanga,” anasema.
Mwape na uzoefu wa mechi za watani wa jadi?
“Nina uzoefu wa kucheza
katika timu yenye mpinzani wa jadi, nimekuwa Orlando Prates, ni wapinzani wa
Kaizer Chiefs, katika msimu wangu mmoja tu nilifunga bao la ushindi kwenye
fainali ya Vodacom Challenge tukishinda 2-1.
Soka ni mchezo wa nafasi, nimekutana
na Simba na nikapata nafasi, nikawafung. Nakumbuka nilipowafunga bao Kaizer Chiefs
wakati nipo Pirates, mashabiki walifurahi sana, walishangilia kwa sababu yangu,
nilifurahi sana, kuwafunga wapinzani wa jadi ni raha sana… nataka niendelee kufanya
hivyo tena na tena nikiwa Yanga,”anasema Mwape.
Mwape anazungumzia fainali za
Kombe la Dunia zilizopita Afrika Kusini, ambako pamoja na Afrika kuwa weneyeji
walishindwa kufika angalau Nusu Fainali kwa kusema kwamba; “Watu weupe
wametuzidi sana, wana kila kitu. Afrika tuna timu, lakini tunahitaji kukaa na
timu ya taifa kwa muda mrefu kambini tucheze pamoja tuzoeane. Drogba akiwa
Ivory Coast hawezi kucheza kama anavyocheza Chelsea, lakini kama timu zitaweza
kuwa na wachezaji angalau kwa miezi miwili mfululizo kambini wakifanya mazoezi
pamoja, tunaweza kusogea mbele,”anasema.
Mwape anavutiwa na mchezaji
gani duniani? “Nampenda Ronaldo Lima,”anamtaja mpachika mabao wa zamani wa
kimataifa wa Brazil.
Katika kucheza kwake kote
soka, mabao mengi zaidi alifunga akiwa Chambishi SC ya Zambia ikimenyana na National
Assembly mwaka 2004, alipiga matatu peke yake, lakini anasema zaidi amekuwa
akifunga hadi mabao mawili kwenye mechi moja.
Mwape ni mshambuliaji wa
staili gani? “Staili yangu ni bull dozer (kunyanyasa mabeki), kasi, kutumia
nguvu, kupiga mashuti, vichwa, Yanga wanaona wenyewe kazi yangu, nitaendelea kupigana
kwa uwezo wangu wote,”anasema.
Davies Robby Mwape alizaliwa
Desemba 5, mwaka 1986, Kitwe, Zambia na alipata elimu ya Msingi katika shule ya
Kawama na sekondari alisoma Mindolo, hadi Kidato cha Tano, zote zipo Kitwe.
Kisoka, Mwape kama walivyo
nyota wengi duniani, alianzia utotoni kabisa akicheza timu ya watoto ya Police Tigers,
iliyokuwa inaundwa na vijana wa umri chini ya miaka 14, mwaka 2003 akasajiliwa
na timu ya Daraja la Kwanza, Kwiza FC aliyoichezea kwa msimu mmoja tu, kabla ya
kuhamia Chambishi FC ya Ligi Kuu mwaka 2004.
Akiwa Chambishi mwaka 2004,
Mwape anasema aliunganishiwa nafasi ya kwenda kufanya majaribio Ufaransa katika
klabu ya Chateroux na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Zambia, Kalusha
Bwalya na akafuzu na kupewa mkataba wa miaka minne.
Hata hivyo, pamoja na uongozi
wa Chateroux kumtajia mkataba utakavyokuwa ikiwemo mishahara posho na
kadhalika, Mwape anasema siku moja akaambiwa chukua barua hii mpelekee Bwalya
Zambia.
“Nikapanda ndege kurudi
Zambia, sikuifungua ile barua kufika nikampa Kalusha, akaniambia atanitafuta.
Hakuwahi kunitafuta tena, ndio nikapata nafasi nyingine Pirates. Lakini baadaye
nikagundua FAZ walitaka fedha nyingi sana kutoka Chateroux, wakaghairi,”anasema
Mwape.
Hata hivyo, anasema hajakata
tamaa ya kucheza Ulaya anaamini kama atafanikiwa kufanya vizuri Yanga kuanzia
ligi ya nyumbani hadi michuano ya Afrika, anaweza kupata nafasi ya kurejea
Ulaya.
Mwape anasema alidumu Orlando
Pirates tangu 2005 hadi 2006 alipohamia Jomo Cosmos
“Pirates walinitoa kwa mkopo
kwenda klabu moja inaitwa FC AK, nilienda lakini sikucheza, kwa sababu hakukuwa
na nafasi ya mchezaji wa kigeni, walikuwa wana wageni watano tayari, wakawa
wanasubri mchezaji mmoja apate uraia ili wanisajili mimi…ndio nikaamua kwenda
Jomo,”anasema.
Alidumu Jomo Cosmos hadi
mwaka 2009 aliporejea Zambia kujiunga na Zanaco, kufuatia mkataba wake kumalizika
nchini humo.
Kwa nini alitemwa Jomo
Cosmos? “Afrika Kusini wamepitisha sera ya kutosajili wachezaji wa kigeni ili
kukuza uwezo wa wachezaji wao. Wachezaji wengi wameondolewa kwenye timu Afria
Kusini na wamekimbilia timu ndogo ndogo ambazo hata maslahi yako chini,”anasema
Mwape, ambaye kutoka Zanaco, alijiunga na Power Dynamos alikocheza nusu msimu
na kujiunga na Konkola Blades ambako baada ya miezi kadhaa, akatua Yanga.
Mwape ana mchango wake katika
tiketi ya Zambia ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006 nchini
Misiri, kwani alicheza mechi zote za kuwania kufuzu chini ya kocha Kalusha
Bwalya, lakini anasema timu ilipofuzu akaumia na kuwa nje ya kikosi.
“Nimechezea timu ya taifa mwaka
2005 na 2006 chini ya Kalusha. Nilicheza mechi za kufuzu 2006, timu ilipofuzu
nikaumia, sikwenda Misri, tangu nimepona sijapata nafasi tena.
Mwape ni mume wa Lucia waliyefunga
naye pingu za maisha mwaka 2005 na wamefanikiwa kupata mtoto mmoja aitwaye Richard,
ambaye ana umri wa miaka sita sasa. Je, atapenda mwanawe acheze soka pia?
“Sitaki kuingilia uhuru wa mwanangu, ataamua yeye mwenyewe kuhusu maisha
yake,”anasema Mwape, ambaye familia yake ipo Kitwe.
Baba yake, Robby Mwape ni
Mhandisi, wakati mama yake Lwini Soneka alifariki dunia Januari mwaka juzi
mjini Kitwe.
Mwape ana kaka yake aitwaye William
Soneka Mwape ambaye aliwahi kucheza soka katika nafasi ya kiungo kwenye klabu
ya Kitwe United.
Huyo ndiye Davies Robby
Mwape, mshambuliaji ambaye hajaripoti kambini kwa maandalizi ya mzunguko wa
pili wa Ligi na Ligi ya Mabingwa, ambayo Yanga itaanza na Zamalek ya Misri.
Je, kuna nini kinaendelea juu
yake na klabu yake? Dar es Salaam, Yanga wanasema anaumwa, yeye anazungumza
kutoka Zambia anasema yupo fiti kabisa. Yetu macho na masikio, tuvute subira.
Tutajua ukweli.
WASIFU WAKE:
JINA: Davies Robby Mwape
KUZALIWA: Desemba 5, 1986
ALIPOZALIWA: Kitwe, Zambia
KLABU YAKE: Yanga
KLABU ALIZOCHEZEA:
2004-2005: Chambishi FC
(Zambia)
2005-2006: Orlando Pirates
(A. Kusini)
2006-2009: Jomo Cosmos (A.
Kusini)
2009: Zanaco (Zambia)
2010: Power Dynamos
(Zambia)
2010: Konkola Blades
(Zambia)
0 comments:
Post a Comment