Nadir Haroub 'Cannavaro' kushoto, mmoja wa wachezaji wa Yanga walio hatarini kufungiwa |
WACHEZAJI zaidi ya watatu wa Yanga, huenda wakafungiwa miezi
mitatu kucheza soka kutoka na kitendo chao cha kumpiga mwamuzi, Israel Mujuni
katika mechi yao dhidi ya Azam iliyopigwa
mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kulala mabao 3-1,
uliingia mushkeli dakika ya 13 baada ya Haruna Niyonzima kupewa kadi nyekundu
kwa kile kilichoelezwa kuzozana na mwamuzi na kumtolea lugha chafu.
Wachezaji ambao rungu la Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ni
dhahiri litawaangukia ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Stephano Mwasika na Nurdin
Bakari wakati Jerry Tegete huenda naye akaangukiwa na hilo baada ya kutaka
kuingia ndani ya uwanja kwa nia ya kumdhuru mwamuzi. Hata hivyo alizuiwa na
wachezaji wenzake wa akiba.
Haruna Niyonzima atakosa mechi tatu kama kanuni zinavyosema.
Hata hivyo, Kamati ya Ligi ya TFF itakayokutana wiki hii, itaamua vinginevyo.
Nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, Athumani Idd 'Chuji',
Omega Seme na Hamisi Kiiza walifanya kazi ya ziada kuwazuia wachezaji hao
pamoja na daktari wa timu, Juma Sufiani.
Wachezaji hao wanabanwa na Kanuni ya 25 ya udhibiti wa
wachezaji kipengele (F) kifungu cha (iii) kinachosema, mchezaji yeyote
atakayemshambulia mwamuzi au kiongozi yeyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa
matusi au kwa kumgusa, ataadhibiwa kwa kufungiwa kwa kipindi kisichopungua
miezi mitatu hadi 12, kufungiwa kucheza michezo kadhaa, kupigwa faini kwa
mujibu wa Kanuni ya 31 au vyote kwa pamoja.
TFF kupitia msemaji wake, Boniface Wambura alisema Kamati ya
Ligi inakutana katikati ya wiki hii baada ya kupokea taarifa ya kamisaa wa
mchezo huo.
Wambura alisema jana kuwa tayari wamepokea taarifa hiyo
kutoka kwa kamisaa wa mchezo na tayari wameiwasilisha kwa Kamati ya Ligi.
"Tayari ripoti imefika kwetu na tulichokifanya sisi ni
kuipeleka kwa wahusika wa mwisho ambao ni Kamati ya Ligi chini ya Wallace Karia
pamoja Godfrey Nyange na wenzake ambapo wataipitia kwa makini kabla ya kuitolea
maamuzi.
"Naamini yote yatakayofanyika yataenda sambamba na adhabu
kwa watu waliohusika na vurugu zile ndani na hata nje ya uwanja," alisema
Wambura.
Mbali na vurugu hizo, kulikuwepo na uharibifu wa mali za
uwanja na baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wakirusha viti uwanjani ikiwa
ni siku chache baada ya Serikali kuagiza Simba kulipa Shilingi5 milioni kwa
kuvunja viti wakati wa pambano lao dhidi ya Kiyovu.
Ukiacha baadhi ya wachezaji hao kuadhibiwa, klabu ya Yanga
italazimika kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na mashabiki wake kwa
kung'oa viti na miundombinu mingine.
Katika hatua nyingine, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima
amewaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka nchini kwa kitendo kilichotokea
mwishoni mwa wiki walipocheza na timu ya Azam na kusababisha vurugu huku akidai
hakumjibu lolote mwamuzi Israel Nkongo
"Nawaomba msamaha mashabiki na wadau wote wa soka hapa
nchini kutokana na vitendo vya vurugu vilivyotokea kwenye mchezo ule na
nawaahidi hakiwezi kutokea tena" alisema Niyonzima.
Aliongeza kusema kuwa mashabiki wasikate tamaa kwani wamekosa
mchezo ule lakini bado wana michezo mingine na kikosi kipo vizuri hivyo
watafanya vizuri kwenye mchezo ujao na kuhakikisha wanatete ubingwa wao.
0 comments:
Post a Comment