Wachezaji wa Barcelona, bingwa mtetezi Ligi ya Mabingwa Ulaya |
MABINGWA watetezi, Barcelona wamepewa kigongo, mabingwa wa Italia,
AC Milan katika droo ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, iliyopangwa
mchana huu.
Vibonde APOEL Nicosia ya Cyprus, timu iliyowahi kumtaka
Joseph Kaniki akiwa Simba SC mwaka 2004 ambayo pia amewahi kuichezea mume wa
mwigizaji Irene Uwoya, Hamadi Ndikumana ‘Katauti’ imepangwa na Real Madrid wakati
Chelsea, timu pekee kutoka Ligi Kuu ya England iliyosalia kwenye michuano hii,
imepangwa na mabingwa wa zamani mara mbili, Benfica ya Ureno.
Bayern Munich ya Ujerumani, ambao Uwanja wao utapokea fainali
ya michuano hii Mei 19, itamenyana na Olympique Marseille ya Ufaransa.
"Ni vuzuri tunaanzia ugenini na tunaweza kujenga msingi
kutoka hapo," alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay, ambaye
timu yake imeitoa Napoli kwa mbinde.
"Ramires na David Luiz watajua zaidi kuhusu Benfica na
pia tunajua zaidi kuhusu Benfica, kwa sababu waliongoza kundi ambalo lilikuwa
Manchester United na timu ni nzuri."
Kocha Msaidizi wa Marseille, Guy Stephan, ambaye timu yake
iliitoa kwa mbinde Inter Milan katika 16, Bora aliiambia L'Equipe TV: "Itakuwa
mechi muhimu sana ambayo itakuja mwishoni mwa msimu wetu. Tutakuwa na wakati
mgumu kuanzia nyumbani.
"Lakini tuna rekodi nzuri, tayari tumeifunga timu ya Ujerumani
msimu huu. Na Borussia Dortmund inaongoza Bundesliga mbele ya Bayern. Pia tulifanya
vitu dhidi ya Inter ambayo tulipata nafasi nyingi dakika za mwishoni."
Barca na Milan tayari zimekutana katika hatua ya makundi msimu
huu na matokeo yalikuwa sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Nou Camp kabla ya ushindi
wa 3-2 kwa Barca kwenye Uwanja wa San Siro wakati timu zote zikiwa
zimekwishafuzu hatua ya mtoano.
Katika Nusu Fainali, Milan au Barcelona timu mojawapi
itamenyana na mshindi kati ya Benfica na Chelsea. Mshindi wa mechi kati ya Bayern
na Marseille atamenyana na Real au APOEL.
Fainali kati ya Real na Barca ni jambo ambalo linatarajiwa
sana. Tena sana.
Mechi za kwanza za Robo Fainali zitachezwa Machi 27 na 28 na
marudiano Aprili 3 na 4. Mechi za kwanza za Nusu Fainali zitachezwa April 17 na
18 na marudiano Aprili 24 na 25.
RATIBA ROBO FAINALI:
Apoel Nicosia v Real Madrid
Olympique Marseille v Bayern Munich
Benfica v Chelsea
AC Milan v Barcelona
NUSU FAINALI:
Olympique Marseille/Bayern Munich v APOEL Nicosia/Real Madrid
Benfica/Chelsea v AC Milan/Barcelona
(Mechi za kwanza robo fainali zitachezwa Machi 27 na 28, marudiano
Aprili 3 na 4, wakati nusu fainali za kwanza zitakuwa Aprili 17 na 18 na
marudiano Aprili 24 na 25- na fainali itakuwa mjini Munich, Mei 19)
0 comments:
Post a Comment