Bin Kleb akimkabidhi jezi Niyonzima |
BAADA ya Yussuf Mehboob Manji, kutangaza kujivua ufadhili wa
klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, wapenzi wa klabu hiyo waliingiwa hofu kidogo
juu ya mustakabali wa klabu yao.
Hali ilikuwa mbaya kati ya 2003 hadi 2006 alipojitokeza
Manji na kuwekeza fedha nyingi kwenye klabu hiyo, hata ikaweza kurejesha hadhi
yake, kusajili wachezaji wa gharama na kuwa mshindani wa kweli.
Lakini hofu iliyotanda kwa kuondoka Manji, imezimwa na
wapenzi kadhaa wa Yanga, waliounda umoja wao na kuamua kwa hali na mali
kuusaidia uongozi wa klabu hiyo katika masuala mazito ya klabu, kama usajili,
maandalizi, malezi ya wachezaji na kadhalika.
Ni orodha ndefu kidogo, lakini DIMBA imefanikiwa kukutana na
mmoja wa wanachama hao ‘waliochizika’ na Yanga, ambaye amechoma mamilioni yake
kibao kuisaidia klabu hiyo.
Huyo ni Abdallah Ahmed Bin Kleb, mfanyabishara kijana ambaye
mtandao wake wa kibiashara umeenea Afrika Mashariki na Kati. Moja kati ya mambo
ambayo kwa sasa wana Yanga wanafurahia ni mataji mawili mfululizo, ubingwa wa
Bara na Kombe la Kagame pamoja na usajili ambao wao wanaamini ni mzuri.
Katika mambo haya huwezi kumuweka kando Bin Kleb, kwani
amechangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwake, akiwa Mjumbe wa Kamati ya
Mashindano ya klabu chini ya Mwenyekiti Seif Ahmed na Mjumbe wa Kamati ya
Usajili chini ya Mwenyekiti Salim Rupia.
Katika mahojiano na DIMBA, Bin Kleb anasema kwamba yeye ni
mpenzi wa Yanga tangu akiwa anasoma shule ya msingi, ingawa baba zake— mzazi na
mdogo wote— ni Simba damu.
“Mimi nilianza kuonyesha mapenzi yangu kwa Yanga tangu
nikiwa mdogo sana, baba mdogo (Ali Bin Kleb) alikuwa mfadhili wa Simba wakati
fulani, alikuwa ananichukua tunaingia na mabenz yetu Uwanja wa Taifa (sasa
Uhuru), mimi nikishuka napanda jukwaa la Yanga, yeye anaenda la Simba.
Hiyo ilikuwa ni miaka ya 1990, wapenzi wa Yanga walikuwa
wanafurahi sana, basi nimeendelea kuwa Yanga hadi leo mimi ni mwanachama na
kiongozi wa kamati mbili,”anasema.
BIN KLEB NI NANI?
Abdallah Ahmed Bin Kleb alizaliwa Septemba 2, mwaka 1973
katika hospitali ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani na alipata elimu yake ya msingi
katika Shule ya Tumbi na Sekondari ya Forest Hill, Morogoro hadi Kidato cha
Sita.
Akiwa mtoto wa kwanza, katika familia yao, Abdallah
alipomaliza Kidato cha Sita moja kwa moja alibeba majukumu ya kusimamia
biashara za baba yake, jambo ambalo amelifanya kwa ufanisi kiasi cha kukuza
biashara hizo za uuzaji mafuta, usafirishaji na utoaji mizigo bandarini.
“Kwa kweli namshukuru Mungu sana, hivi sasa sisi ni miongoni
mwa wafanyabiashara wanaofahamika nchi hii,”anasema Abdallah ambaye alisomea
pia masomo ya biashara.
BIN KLEB NA SOKA:
Anasema soka alianza kuipenda tangu angali mdogo akiwa
anasoma Shule ya Msingi na alikuwa akicheza winga ya kulia wakati huo hadi
anafika sekondari.
Anasema kwamba akiwa Kibaha pamoja na kuchezea timu ya Mwendapole
FC alikuwa akiifadhili pia, lakini baadaye ukatokea mtafaruku akaenda kuanzisha
timu yake mwenyewe, National FC.
Anasema anakumbuka aliwahi hadi kumwalika mshambuliaji wa
zamani wa Yanga, Vaal Professionals ya Afrika Kusini, FC Zurich ya Uswisi, Stade
Rennais, AS Monaco za Ufaransa, AS Roma ya Italia, Blackburn Rovers ya England
na Galatasaray ya Uturuki, Nonda Shabani aichezee ‘ndondo’ timu yao hiyo.
“Ilikuwa mwaka 1995, tulimualika Nonda na Monja (Liseki)
wakati huo akiwa Sigara, waliichezea kwenye mashindano fulani hivi tukachukua
Kombe, lakini timu haikudumu kutokana na mimi kujikita kwenye
biashara,”anasema.
Abdallah anasema kwamba lakini hadi leo anafanya mazoezi na
kucheza mechi za maveterani, kwa kuwa soka ipo kwenye damu yake.
BIN KLEB NA YANGA:
Anasema alikuwa mpenzi wa kawaida tu wa Yanga miaka ya 1980
enzi hizo timu yao ikiundwa na wakali kama Ahmad Amasha, Charles Boniface
Mkwasa, Juma Mkambi na wengineo, lakini baadaye akajikuta mapenzi yanazidi,
kutokana na upinzani aliokuwa akiupata kutoka kwa wazazi wake.
“Baba yangu mzazi na baba yangu mdogo walikuwa Simba sana,
sasa ilikuwa Yanga ikifungwa wananitania sana, na mimi ndio nikaweka dhamira
nikikua nikawa na kipato nitaisaidia Yanga, na kweli sasa hivi nasaidia timu
ninayoipenda,”anasema.
Anasema walianza kama wapenzi wa Yanga waliounda umoja wao
kwa ajili ya kuisaidia timu yao chini ya uongozi wa Imani Madega, kwa
kuchangishana fedha na kuwapa wachezaji au viongozi wahudumue timu.
Anasema uongozi wa Lloyd Nchunga ulipoingia madarakani
akateuliwa kwenye Kamati mbili, ya Mashindano na Usajili na anashukuru kazi
zote amezifanya vizuri.
“Tulianza kwa kuchukua Ngao ya Jamii tukiifunga Simba kwa
penalti, tukaingia kwenye Ligi tukafanikiwa kuipokonya Simba ubingwa na juzi
tumechukua Kombe la Kagame, tukiifunga Simba pia,”anasema.
Abdallah anasema kwamba Novemba mwaka jana aliteuliwa kwenye
Kamati ya timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na anashukuru pia
huko aliiwezesha timu kutwaa ubingwa wa Challenge, kwa mara ya kwanza tangu
itwae mara ya mwisho mwaka 1994.
Anasema Yanga ingeweza kuwa mataji manne kwenye kabati lake
mwaka huu kama si mgogoro baina ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nchunga na Makamu
wake, Davis Mosha kuiathiri timu hadi ikafungwa na Simba mabao 2-0 kwenye
Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
USAJILI BOMBA JANGWANI:
Abdallah anazungumzia usajili wa Yanga msimu huu na kusema
kwamba ni mzuri mno, kiasi kwamba anaweza kuufananisha na usajili wa mwaka
1994, kikosi kilichokuwa na wakali kama Riffat Said, Issa Athumani, Nico
Bambaga, Method Mogella, Steven Mussa, Said Mwamba ‘Kizota’ (wote marehemu),
Constantine Kimanda, Ngandou Ramadhan, Edibily Lunyamila, Mohamed Hussein,
Sekilojo Chambua, Fumo Felician, Mtwa Kihwelo na wengineo.
Kikosi anachojivunia Abdallah Bin Kleb msimu huu ambacho
kimebeba Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo itwae mara ya
mwisho mwaka 1999 ni hiki; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Godfrey Taita, Nurdin Bakari ‘Tshabalala’,
Davies Mwape, Kenneth Asamoah, Kiggi Makassy, Bakari Mbegu, Rashid Gumbo,
Julius Mrope, Jerry Tegete, Kiiza Hamisi, Shaaban Kado, Said Mohamed, Freddy
Mbuna, Geoffrey Bonny, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Pius Kisambale, Idrisa
Rajab, Stefano Mwasyika, Abuu Ubwa, Shamte Ally, Job Ibrahim na Salum Telela.
Anasema
kikosi hiki kimeonyesha mwanzo mzuri kwa kutwaa Kombe la Kagame, kwani taji
hilo lina maana kubwa Yanga.
“Unajua
Simba walikuwa wamechukua hilo Kombe mara sita, sasa kama wangechukua tena
ingekuwa mara ya saba, ina maana wangezidi kutuacha mbali na kutukatisha tamaa,
ila kuchukua kwetu ina maana katika rekodi wao wanatuzidi mara mbili tu sasa.
Lengo
letu ni kuhakikisha tunachukua tena na tena Kombe hilo hadi tuwafikie na
kuwapita Simba kama tunavyowazidi kwenye Ligi ya Bara,”anasema.
Anasema
kutokana na kikosi hicho, wamedhamiria kutwaa ubingwa wa Bara na kufika hatua
ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani na ili kutimiza azma hiyo
watahakikisha wanaiandaa vizuri timu na kuihudumia pia.
“Tumeweka
kipaumbele katika suala la maslahi ya mchezaji, tutahakikisha kila mchezaji
anatekelezewa haki zake zote za msingi zilizomo kwenye mkataba wake, sisi
tunataka mataji tu,”anasema.
USAJILI
WA NIYONZIMA FABREGAS:
Akizungumzia usajili wa Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ kutoka
APR ya Rwanda, Bin Kleb anasema kwamba baada ya kocha kupendekeza wachezaji
anaowataka, Wajumbe wa Kamati ya Usajili waligawana majukumu, naye kwa kuwa ana
ofisi zake Rwanda, akachukua jukumu la kumsajili mchezaji huyo.
“Kocha alisema ni ngumu kumtoa Haruna APR, alikuwa haamini
kabisa. Hata wajumbe wenzangu wa Kamati walikuwa hawaamini kabisa kama ninaweza
kufanikisha hilo,”anasema.
Bin Kleb anasema ‘aliingia kazini’ na hatimaye akafanikiwa
kumpata Niyonzima na kumsainisha mkataba na ili kuwadhihirishia Wajumbe wenzake
kwamba amefanikisha zoezi hilo pamoja na kuwatumia nakala za mkataba, pia
aliwatumia picha akiwa na mchezaji huyo anasaini mkataba na kumkabidhi jezi
namba nane ya Yanga.
Hata hivyo, Bin Kleb anasikitika baada ya kusajiliwa
mchezaji huyo, baadhi ya vyombo vya habari vimeibuka na maoni kwamba usajili
wake haukutokana na ushauri wa kocha bali na maamuzi ya viongozi.
“Huyu ni kati ya wachezaji ambao kocha alipendekeza
wasajiliwe, hata wengine wote waliosajiliwa na kuachwa ni mapendekezo ya kocha.
Kati ya wachezaji ambao kocha alipendekeza na tukawakosa ni Mussa Mgosi, Juma
Kaseja, Obadia Mungusa na Mohamed Banka, yaani hawa wote wamo kwenye orodha ya
kocha, sasa inakuwaje watu wanaibuka na maoni ya uongo?”anahoji Bin Kleb.
Anasema maoni ya aina hiyo yanalenga kuwavuruga Yanga katika
wakati huu na ameomba wapenzi wa klabu hiyo wayapuuze.
UBABE WA YANGA KWA SIMBA:
Bin Kleb anasema anafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya
Yanga, kwani mbali na kutwaa mataji matatu, lakini wamemaliza msimu wakiwa
wamewafunga wapinzani wao wa jadi, Simba mara tatu, kutoka sare moja na
kufungwa moja.
“Tuliwafunga katika Ngao, tukawafunga kwenye ligi mechi moja
na kutoka sare moja, tumewafunga pia katika Kombe la Kagame, ni raha sana hii,
wao walitufunga Kombe la Mapinduzi tu, tena kwa sababu tulikuwa tuna mgogoro,
hatukujipanga vizuri,”anasema.
Bin Kleb anasema kwamba matokeo ya Kombe la Mapinduzi
yamemfundisha kwamba migogoro si mizuri katika klabu, hivyo amewataka wapenzi
na wanachama wote wa Yanga kuhakikisha hawawi chanzo cha migogoro kwenye klabu
hiyo.
Aidha, anatoa wito kwa wana Yanga wote kwamba wasikae
kusubiri klabu iwafanyie kitu, bali wanapaswa sasa kufikiria wataifanyia nini
klabu yao.
Ana ndoto za kuwa kiongozi wa Yanga siku moja? “Hapana,
hapana kabisa, mimi nitaendelea kuwa nasaidia timu yangu tu, lakini uongozi
hapana kabisa,”anasema.
Naam, huyo ndiye Abdallah Ahmed Bin Kleb, mwanachama wa
Yanga aliyefanikisha usajili wa Fabregas Jangwani.
0 comments:
Post a Comment