SERIKALI ya Zambia imewapa wachezaji wa timu ya taifa ya
nchi hiyo kiasi cha dola za Kimarekani 59,000 kila mmoja kwa kutwaa ubingwa wa
Kombe la Mataifa ya Afrika Jumapili, alisema Waziri wa Michezo wa nchi hiyo
jana.
“Serikali imempa kila mchezaji dola za Kimarekani 59,000, na
hiyo ni nje na mashirika au vikundi mbalimbali vitakavyoamua kuwapa. Hizi ni
fedha kutoka serikalini,” alisema Chishimba Kambwili leo na kukaririwa na
Radio ya taifa Zambia.
Zambia iliifunga Ivory Coast kwa penalti 8-7 baada ya sare
ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Fainali hiyo ilipigwa Mji Mkuu wa Gabon, Libreville, ambako
ndiko ndege iliyokuwa imebeba wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa ya Zambia
ilianguka mwaka 1993, kwenye pwani ya bahari ya Atlantic na kusababisha vifo
vya wachezaji wote 30, viongozi na wafanyakazi wa ndege.
Mabingwa hao, Chipolopolo walirejea nyumbani juzi na
kupokewa kwa shangwe mjini Lusaka na umati wa watu zaidi ya 200,000 ukiwalaki.
Ushindi huo pia utawafikisha wachezaji katika makaburi ya
wachezaji wa Zambia waliofariki ajalini mwaka 1993, ambako Rais Michael Sata alitarajiwa
kuongoza ibada maalum ya heshima kwa mashujaa hao wa zamani wa taifa hilo.
0 comments:
Post a Comment