Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) ilikutana Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kufanya uamuzi
kwa ajenda mbalimbali ikiwemo Marekebisho ya Katiba za Wanachama wa TFF, na pia
ushauri wa kisheria ulioombwa kwake na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Uamuzi uliofanywa kwa wanachama wote 40 wa TFF ni ufuatao;
wanachama wote wanatakiwa kufanya marekebisho kwenye katiba zao katika maeneo
matatu kwa mujibu wa maelekezo ambayo TFF ilitoa mwaka jana.
Maeneo hayo ni sifa za wagombea uongozi ambapo kwenye
kipengele cha elimu ni lazima iwe kuanzia kidato cha nne, kutopeleka masuala ya
mpira wa miguu katika mahakama za kawaida na kamati zao za uchaguzi kufanya
kazi chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Hivyo hakuna mwanachama yeyote wa TFF anayeruhusiwa kufanya
uchaguzi kwa sasa kama katiba yake ina
upungufu au inakwenda kinyume na maelekezo kuhusu maeneo hayo matatu.
Kamati imetoa hadi Juni Mosi mwaka huu kwa wanachama ambao
katiba zao zina upungufu katika maeneo hayo wawe wamefanya marekebisho ndiyo
waendelee na uchaguzi kwa wale ambao muda wa uchaguzi umefika.
Ushauri wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kuwa katiba zote za wanachama ziwe na vitu
hivyo vitatu.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
0 comments:
Post a Comment