KOCHA wa zamani wa muda wa Chelsea, Guus
Hiddink ameteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi, anayochezea mwanasoka bora wa kihistoria Afrika, Samuel Eto'o.
Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 65, aliyewahi kuikochi timu ya taifa ya Urusi, amekubali mkataba wa kuifundisha timu hiyo hadi mwishoni
mwa msimu wa 2012-2013, ingawa klabu hiyo ilihusishwa pia na mpango wa kumtwaa kocha aliyeachia ngazi England, Mtaliano Fabio Capello. Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Yury Krasnozhan, alijiuzulu Jumatatu baada ya kuvuna pointi mbili tu akiwa kazini Anzhi.
"Nina furaha kuikubali fursa hii,"alisema Mholanzi huyo.
Hiddink aliiongoza Chelsea kutwaa Kombe la FA mwaka 2009 alipokuwa akiifundisha kwa muda klabu hiyo, akimpokea Luiz Felipe Scolari aliyetupiwa virago Februari mwaka 2009.
Hivi karibuni alikuwa akiifundisha Uturuki, lakini akaachia ngazi baada ya timu hiyo kukosa tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2012.
0 comments:
Post a Comment