Hii ni mechi kati ya Simba na Yanga, iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana mwaka 1974. Hapa kipa Athumani Mambosasa (marehemu) anaruka kudaka mpira mbele ya Kitwana Manara.
SHIRIKISHO la Kimataifa la Soka (FIFA) limetoa dola za Marekani 500,000 kwa ajili ya mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye moja ya viwanja vya Mkoa wa Mwanza. Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo wakati akizungumza wa wadau wa michezo ofisini kwake jana ambapo alisema fedha hizo zimetolewa zikiwa na masharti. Aliyataja masharti hayo kuwa ni pamoja na kukubali kuongeza gharama iwapo fedha hizo hazitatosheleza na pia uwanja utakaowekewa nyasi hizo utumike kwa kuendeleza mchezo wa soka. Alisema baada ya kupokea barua hiyo ya FIFA, Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilikubali uwanja wa Nyamagana kuwekewa nyasi hizo na kwamba wapo tayari kuongeza gharama iwapo fedha hizo hazitatosheleza. Ndikilo alisema Serikali ya Mkoa ipo tayari kushirikiana na wana Mwanza kuhakikisha kunakuwa na kiwanja kizuri cha kuendeleza soka hapa mkoani. Uwanja wa Nyamagana utakuwa wa nne kuwekewa nyasi hizo za bandia kwa hapa nchini ambapo tayari viwanja vya Uhuru na Karume vya jijini Dar es Salaam na Migombani cha Zanzibar vimewekewa nyasi hizo. “Hii ni nafasi nzuri kwa wana Mwanza kuhakikisha mchezo wa soka unarudi kwenye nafasi yake kwa kasi kama ilivyokuwa siku za nyuma nami niliahidi nilipofika mkoani hapa kuwa nitahakikisha michezo inakuwa kwenye nafasi nzuri,” alisema Mkuu wa Mkoa. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Jackson Songora alisema maandalizi yote juu ya mradi wa uwekaji nyasi bandia yamekamilika kwa upande wa Mkoa na wanaosubiriwa kwa sasa ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza utekelezaji. | ||
0 comments:
Post a Comment