BARAZA la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC) limemsimamisha bondia Muingereza mwenye asili ya Zimbabwe, Dereck Chisora jana kufuatia kitendo cha utovui wa nidhamu alichoonyesha kwa kupigana na bingwa wa zamani wa WBA, David Haye baada ya pambano lake dhidi ya Vitali Klitschko mjini Munich, Ujerumani.
WBC ilitoa tamko hilo na kulaani kitendo cha Chisora baada ya pambano la Februari 18, ikisema “Inachukuliwa kama moja ya matukio mabaya ya utovu wa nidhamu kufanywa daima na bondia wa kulipwa.”
Chisora alimpiga kibao Klitschko wakati wa kupima uzito kabla ya pambano lao la kuwania taji la WBC uzito wa juu, kisha akamwagia maji kaka yake, Wladimir usoni kabla ya kuanza kwa pambano hilo.Baada ya pambano kumalizika akipigwa kwa pointi, alimgeukia Haye katika Mkutano na Waandishi wa Habari mbele ya watu na kuanza kupigana na Muingereza mwenzake.
WBC imesema pia itampiga faini kali Chisora ambayo hata hivyo itatajwa baadaye.Chisora sasa ataondolewa kwenye orodha ya mabondia wa WBC na adhabu yake inaanzia siku ya pambalo lake. Lakini adhabu hiyo haimzuii kupigania mataji ya vyama vingine kama WBA au IBF.
0 comments:
Post a Comment