Wachezaji Stars wakiwasili jana Uwanja wa ndege, Julius Nyerere Dar es Salaam.
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilirejea nchini jana, ikitokea Ivory Coast ilikokuwa ikishiriki Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), huku wachezaji Haruna Moshi 'Boban' na Athuman Idd ‘Chuji’ wakiwa kituko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa mapokezi.
Wachezaji hao inadaiwa walipishana maneno na Kocha Mkuu wa Stars, Mbrazili Marcio Maximo, wakati wakiwa nchini Ivory Coast.
Timu hiyo iliwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam saa tatu asubuhi na kupokewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, ambapo Iddi na Moshi ‘Boban’ waligeuka sinema mara baada ya timu kuwasili.
Wachezaji hao walionekana kuwakwepa wanahabari mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, ikiwa ni pamoja na kutokea mlango tofauti na wenzao ambao walitokea kwenye lango la wageni maalumu (VIP), wakati wachezaji hao walipita katika mlango wa kutokea wa wageni wa kawaida wanaowasili. Waandishi wa habari walipogundua hilo na kuwafuata kutaka kuzungumza nao, wachezaji hao waligoma kuzungumza sababu za kutokuwa pamoja na wenzao, huku kila mmoja akionyesha kutokuwa tayari kuzungumza zaidi juu ya suala hilo na kwenda moja kwa moja kwenye gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa kwenye maegesho ya magari ya uwanja huo na kuingia. Baada ya kuingia kwenye gari hilo, wanahabari waliokuwa na uchu wa kujua nini kinaendelea kutokana na hali hiyo ya kuwakimbia na kutopanda gari la timu pamoja na wenzao, waliwafuata wachezaji hao kwenye gari lenye vioo vya giza (tinted) , ndipo Iddi alipofungua mlango na kusema asingekuwa tayari kusema lolote kwa leo. “Eeh bwana hapa hazungumzi mtu kitu, kama mnataka tuzungumze subirini hadi kesho (leo), ndipo tutazungumza,” alisema na kufunga mlango wa gari hilo. Licha ya Chuji na Haruna, wengine ambao hawakupita mlango wa VIP ni Kelvin Yondani, lakini mchezaji huyo alirudi kuungana na wenzake. Wakati hayo yakiendelea, wachezaji wengi wa Stars walikuwa wakipiga picha za pamoja na viongozi waliokuwa kwenye msafara pamoja na Bendera aliyefika kuwapokea na baadaye viongozi hao pamoja na kocha kuzungumza na wanahabari. Akizungumza uwanjani hapo leo, Maximo alisema michuano ya CHAN imeiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika na mafanikio mazuri kwa kipindi hiki hasa kwenye fainali za kwanza za michuano hiyo na kinachotakiwa sasa ni kujaribu kuendelea kuwa hapo kwa kufanya vizuri zaidi. “Endapo tutafuata programu zetu za kukuza soka letu kikamilifu, tutakuwa kwenye njia sahihi ambayo itatufikisha kule ambako tunahitaji kufika,” alisema Maximo. Pia alisema kesho atatangaza kikosi cha Stars ambacho kitacheza mchezo wa Kimataifa wa kirafiki na timu kutoka Marekani ya Vancouver Whitecaps, kikosi ambacho hawatakuwemo wachezaji wa Yanga na pia kitajumuisha wachezaji wengi chipukizi. Kwa upande wake, Bendera aliipongeza Stars kwa kazi nzuri waliyofanya CHAN, kwa kuonyesha uwezo kwa kucheza mpira wa ufundi, lakini bahati haikuwa yao. Pia alisema pamoja na kushindwa kwa timu hiyo kufuzu kucheza nusu fainali, serikali haijakata tamaa na itaendelea kujipanga zaidi kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana. Naye nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema pamoja na malengo waliyowaahidi Watanzania kutotimia, walijitahidi kwa uwezo wao kutetea taifa na matokeo yaliyopatikana ni sehemu ya mchezo, na kuishukuru serikali, wadau na mashabiki wote kwa kuwaunga mkono. Stars iliaga kwenye michuano hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia na kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya CHAN kutoka Kundi A, ambalo lilikuwa na timu za Zambia na Senegal zilifuzu kwa hatua hiyo zikiwa na pointi tano, Stars ilikuwa na pointi nne ikishika nafasi ya tatu, huku Ivory Coast ikishika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja. Wakati huo huo, akizungumza baadaye leo jioni kwa simu, Chuji alisema walichokifanya ni kuepuka maswali kwa waandishi wa habari, lakini pia kuna mambo ambayo hayakuwa mazuri kwa upande wao katika safari, hivyo hawakuona sababu ya kujichanganya na wenzao. “Yapo mambo mengi ya msingi naamini Ijumaa (kesho) tutakuwa na la kuzungumza, inakera sana, sisi ni watu wazima, hatupendi matatizo, ila ukweli unabaki kuwa kuna matatizo makubwa. “Naomba vuteni subira tutasema kila kitu kilichotokea ni suala la muda tu, hakuna tutakachoacha, “ alisema Chuji. Naye Anastazia Anyimike anaripoti kuwa Maximo anatarajia kwenda mapumziko ya wiki tatu nyumbani kwao Brazil. Akizungumza mjini Abidjan juzi kabla ya Stars kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam, Maximo alisema atachukua mapumziko ya wiki tatu kabla ya kurejea kuendelea na kazi. Kocha huyo alisema anatarajia kuzungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu mkataba wake ambao unamalizika Julai. Alisema atakuwa na mazungumzo na TFF kujadili iwapo ataongeza mkataba au la, baada ya kurejea mapumzikoni.
0 comments:
Post a Comment