MSHABIKI wa Simba leo watakuwa na kila sababu ya kuwashangilia watani wao jadi, Yanga wakati watakapomenyana na Kagera Sugar ya Bukoba kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam, maarufu kama Shamba la Bibi.
Kagera Sugar inayowania nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara itaipiku Simba iwapo leo itaifunga Yanga. Ikumbukwe mshindi wa pili, hushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), wakatyi bingwa ambaye tayari ni Yanga atashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itashuka dimbani joni ya leo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mara mbili mfululizo na Kagera, kwanza ni 3-1 kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi hiyo msimu uliopita na 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi hiyo msimu huu.
Kagera itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbvu ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Prisons ya Mbeya ambao walinyukwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Lakini pamoja na kupoteza mchezo dhidi ya Prisons, Kagera inajivunia jeuri yao ya kuzitesa timu vigogo kila inapokumbana nazo na leo itakuwa ikiwania kuendeleza ubabe wake mbele ya Yanga ikitaka kuwakumbushia kipigo cha mabao 3-1 katika mchezo wa duru la kwanza uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Mshambuliaji wake aliyepachika mabao mawili katika mchezo huo, Philip Lando hayumo tena kwenye kikosi cha Kagera baada ya kuhamia Azam FC kwenye usajili wa dirisha dogo, lakini itakuwa ikiwategemea zaidi mshambuliaji wake Mike Katende, Paul Ngwai na kiungo mchezeshaji Paul Kabange kuhakikisha inaibuka na pointi tatu. Kwa upande wa Yanga ambayo pamoja na kuwa tayari imeshatangaza ubingwa wa msimu wa 2008/09 haitokubali kufanywa ngazi na Kagera na itataka kulinda heshima yake, ikiwa ni pamoja na kulipa kisasi cha kipigo cha mzunguko wa kwanza. Yanga pia itakuwa ikiutumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yake ya mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri utakaofanyika Jumamosi wiki ijayo. Mbali na Yanga na Kagera Sugar, mechi nyingine za ligi hiyo zitachezwa mjini Morogoro kati ya Villa Squad na Mtibwa Sugar, ambao nao wanaifukuzia kwa karibu nafasi hiyo ya pili wakiwa na pointi 25, wakisubiri Simba na Kagera zenye pointi 27 ziteleze.
0 comments:
Post a Comment