Kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki CHAN baada ya kurejea nchini, Nizar Khalfan ni wa pili kushoto waliosimama mbele
MWANDISHI wa kimataifa, Samm Audu aliyekuwa akifuatilia michuano ya kwanza ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) iliyofanyika kwa wiki mbili nchini Ivory Coast.
Wachezaji hawa ndio wenye uwezekano mkubwa kuwa wamepata mikataba ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Abdul Rahim Ayew (Ghana)
Ni mchezaji wa kiwango cha juu anayeweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, kijana huyu ni mtoto wa kwanza wa mwanasoka maarufu Afrika, Abedi Pele. Aliibuka na kuwa gumzo kimataifa baada ya jitihada zake kufanikisha timu yake ya Ghana kupata pointi muhimu katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Zimbabwe. Amekuwa mchezaji wa vikosi vya Ghana vya U-17, U-20 na U-23. Akiwa na umri wa miaka 23, ana nafasi kubwa ya kuuza kipaji chake Ulaya.Mdogo wake, Andre Dede Ayew, aliiongoza Ghana kutwaa taji la Afrika kwa Vijana michuano iliyofanyika Rwanda mwezi uliopita na sasa uwezo aliouonyesha Rahim umedhihirisha kuwa soka limo ndani ya damu ya kina Ayew.
Tresor Mabi Mputu (DR Congo)
Mshambuliaji huyu anayevutia amewahi kufanya majaribio ya kuchezea Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza na amekuwa akihusishwa na taarifa za kujiunga na vilabu kadhaa vya Ufaransa na Ubelgiji tangu alipoibuliwa na TP Mazembe mwaka 2007 kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Ana kipaji cha kutisha na amefanya mambo makubwa wakati wa Ligi ya Mabingwa mwaka juzi alipofunga mabao tisa na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Kijana huyo wa miaka 23 ni mchezaji mwingine wa kimataifa aliyecheza michuano ya wachezaji wa ndani mwaka huu, wakati mwaka 2006 alikuwapo kwenye fainali za Mataifa ya Afrika huko Misri. Kocha wa zamani wa DRC, Claude Le Roy, amekuwa akimwita Samuel Eto'o ajaye.
Philip Marufu (Zimbabwe)
Mshambuliaji wa Dynamos aliyetoa mchango mkubwa wakati timu yake ilipofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana. Alifunga mabao mawili kwenye CHAN, ingawa Zimbabwe ilitolewa katika raundi ya kwanza.
Khalfan Nizar (Tanzania)
Kiungo huyu wa kazi (enterprising midfielder) amewahi kucheza soka la kulipwa ughaibuni nchini Kuwait, lakini sasa yuko nyumbani. Alikuwa na mchango mkubwa kwa nchi yake kiasi cha kukaribia kuingia raundi ya mwisho ya michuano ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2010, akiwa amecheza mechi tano na kufunga bao moja. Kwa vyovyote sasa njia ni nyeupe kwenda nchini China.
Traore Mamadou Baila (Senegal)
Nyota huyu mshambuliaji wa Port Autonome ni mdogo wa nyota wa zamani wa kimataifa wa Senegal, Omar Traore. Aliiwezesha Senegal kuifunga Tanzania kwenye michuano ya CHAN. Aling’ara katika safu ya ushambuliaji ya Senegal nchini Ivory Coast na kuonyesha kuwa mambo kwake bado mabichi. Ndoto zake za kucheza Ulaya zipo baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye CHAN.
Younes Shibani (Libya)
Mwanasoka huyu wa Al-Ittihad ya Tripoli ambaye ni mlinzi mfungaji wa mabao anafahamika zaidi kwa utaalamu wake wa kuipiga mipira iliyokufa. Alisababisha kupatikana kwa bao katika mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Ghana wakati wa CHAN. Cha kufurahisha zaidi, alifunga mabao manne wakati wa kampeni za timu yake katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2007. Ni mchezaji wa kimataifa akiwa ameichezea timu ya taifa mara 40 na kufunga mabao manne.
Akiwa na miaka 27 hakuna uwezekano mkubwa wa kucheza soka Ulaya kwa sasa, lakini bado anaweza kwenda hata Asia ingawa inakubalika kuwa wachezaji wa Libya si mara nyingi kutoka nchini mwao.
Given Singuluma (Zambia)
Mshambuliaji huyu hatari wa Zanaco atakayetimiza miaka 23 mwezi Julai, anaifahamu sana njia sahihi ya kulisogelea lango adui na alihakikishia watu suala hili kwa kufunga mabao matatu peke yake kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Ivory Coast.
‘Jangili’ huyu wa kufumania nyavu, anayetegenea sana msaada wa viungo wa timu yake, amewahi kukataliwa na timu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) iitwayo Bay United. Lakini kijana huyu anayeitwa kwa utani 'Freedom' kutokana na mapenzi yake kwa muziki wa Akon wa Senegal, anakila sababu ya kucheza soka nje ya nchi baada ya michuano hii ya CHAN.
Ends
0 comments:
Post a Comment