KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic anaamini staili yao ya kubadilika kama kinyonga inaweza kumsaidia kuwasimamisha mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly, mjini Cairo, Jumapili wiki hii katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mahojiano maalum na DIMBA, juzi usiku hoteli ya New Afrika, anapoishi Mserbia huyo, alisema kwamba Yanga ina mifumo mitatu ambayo huitumia kulingana na wapinzani wao walivyo, hivyo Ahly watakuwa na wakati mgumu sana siku hiyo.
“Kama mpira wa kasi, Yanga tunauweza, mpira wa kutulia tunauweza, pasi fupi fupi tunagonga, ndefu tunapiga, kwa kweli hivi sasa sina hofu kabisa na hiyo mechi. Zaidi ninawatakia kila la heri wachezaji wangu katika mechi hiyo,”alisema Kondic.
Aliitaja mifumo hiyo anayojivunia kuwa ni 4-4-2, 3-5-2 na 4-3-3 ambayo yote wachezaji wanaimudu vyema na kwamba anashukuru katika mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Vancouver Whitecaps, mipango yake ilitimia.
“Kama utaona leo (juzi), nimechezesha mshambuliaji mmoja tu, nilikuwa na mawinga wawili, lakini siku nyingine hatuchezi hivyo. Niliitumia mechi hii kujaribu kuwaweka pamoja wachezaji ambao hawajacheza pamoja kwa muda mrefu.
Cannavaro na Owino, hawajacheza pamoja muda mrefu, lakini wamecheza vizuri na kuelewana, siwezi kukuambia kila kitu, haya ni mambo ya kiufundi, hizi ni silaha, kwa ufupi mechi hii imenipa mwanga wa nini nakwenda kukifanya Cairo,”alisema.
Alisema wachezaji 20 aliowateua kwa safari ya Cairo ni ambao wanaweza kucheza mfumo wowote, wazoefu na wameiva tayari kupambana na timu bora na kupata matokeo mazuri.
“Sikuwa na Ngassa (Mrisho) leo wala Ambani (Boniphace), niliwapumzisha, Ambani ndio aliwasili jana kutoka China (alienda kwenye majaribio) na Ngassa alirejea kutoka Ivory Coast (alikuwa na timu ya taifa) akiwa ana maumivu kidogo.
Lakini wote wapo kwenye mipango yangu, mwingine ni Geoffrey Bonny, naye hakuwa fiti asilimia mia moja, sikumtumia kabisa, ila naye yupo kwenye mipango yangu,”alisema Kondic.
Wachezaji ambao wanatarajiwa kupeperusha bendera ya Yanga Cairo ni makipa Obren Curkovic na Juma Kaseja, mabeki Wisdom Ndlovu, Shadrack Nsajigwa, Fred Mbuna, George Owino, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Nurdin Bakari, viungo Abdi Kassim, Mrisho Ngasa, Amir Maftah, Athumani Iddi ‘Chuji’, Shamte Ally, Kigi Makasi na Geoffrey Bonny wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Boniphace Ambani, Vincent Barnabas, Ben Mwalala na Mike Barasa.
Walioachwa ni Iddi Ally Mbaga, Maurice Sunguti ambaye hajasailiwa kwenye michuano hiyo, Gaudence Mwaikimba, Castory Mumbara, Razack Khalfan, Ally Msigwa, Hamisi Yussuf, Abubakar Mtiro na Steven Marashi.
Kondic alisema kwamba Yanga itafanya mazoezi kwa mara ya mwisho leo asubuhi na jioni kabla ya kuondoka kesho. “Jumatano ndio nitaangalia kwa mara ya mwisho hali za wachezaji, kama kutakuwa na mabadiliko au la”alisema.
Miongoni mwa mambo ambayo anakwenda kuyafanyia kazi leo ni kuhakikisha kwamba nafasi wanazopata wanatumia kwa wingi, kwani kwenye mchezo na Whitecaps pamoja na kuibuka na ushindi wa 3-0, lakini wangeweza kufunga zaidi ya idadi hiyo kama umakini ungekuwa mkubwa.
“Haya ni mashindano makubwa, nataka wachezaji wangu wawe makini zaidi, wawe na malengo, tunataka tufanye maajabu na tuweke rekodi nzuri, hadi sasa nafurahi naelekea kuipa Yanga taji la pili la ubingwa wa Tanzania,”alisema.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Cairo International, Jumapili kumenyana na Al Ahly katika mchezo wa kwanza, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment