KIUNGO wa klabu ya Simba ya Dar es salaam, Haruna Moshi ‘Boban’, (pichani kulia) amesema licha ya kufungwa na Mtibwa Sugar 1-0 Jumapili iliyopita mjini Morogoro, wataendelea kupigana kwa nguvu zao zote, lengo likiwa ni kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza na DIMBA kwa simu juzi, alisema kipigo hicho kimezidi kuongeza upinzani katika kuwania nafasi ya pili. Kwa sasa mbali na Simba, Mtibwa, pia inaweza kuchukuliwa na Kagera Sugar na JKT Ruvu. Timu zote za Ligi Kuu, zimekwisha kukata tamaa ya ubingwa, kutokana na Yanga kuwa imekwisha kujikusanyia pointi kibao. Kabla ya kumenyana na Toto jana, tayari ilikuwa ina pointi 43.
“Tutajitahidi kushinda michezo yetu iliyobaki, sisi kama wachezaji hatujakata tamaa, timu nyingine ambazo zinataka nafasi hiyo sisi hatuziangalii, tunajipanga kuhakikisha tunashika nafasi hiyo,” alisema Boban.
Simba, inayonolewa na Mzambia, Patrick Phiri, inaweza kufikisha pointi 42, iwapo ‘itajaaliwa’ kushinda mechi zake zote tano zilizobaki, kuanzia Jumapili hii dhidi ya Azam FC inayofundishwa na kocha wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi, Neider dos Santos wa Brazil.
Lakini Kagera ndiyo inaonekana kutishia zaidi uwezekano wa Simba kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani, kutokana na kuwa na uwezo wa kutimiza pointi 45, iwapo itashinda mechi zake zote zilizobaki kuanzia jana dhidi ya Prisons mjini Mbeya.
Madega amtetea kipa wake Mzungu
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Imani Madega, amesema kwamba kipa Obren Curkovic analazimika kuwa karibu na makocha wa timu hiyo, kwa sababu ndio pekee anaoweza kuzungumza nao kwa kuwa wanatoka nchi moja, Serbia.
Madega alikuwa akizungumzia madai ya makocha wa klabu hiyo, chini ya Dusan Kondic na wasaidizi wake, Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan kuwa karibu mno na kipa huyo.
“Kosa tulilolifanya ni kuruhusu msafara mzima wa timu yetu kufikia katika hoteli moja (Cairo), jambo ambalo liliwafanya baadhi ya watu wasiojua mazingira ya kambi, kuibuka na maneno yanayosababisha ionekane kulikuwa na vitendo vya hujuma, kitu ambacho si cha kweli,” alisema Madega, alipozungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam.
Alisema lilikuwa ni jambo la kawaida kwa Curcovic kuondoka na Kondic, kwa kuwa kipa huyo hana mtu wa karibu wa kuzungumza naye zaidi ya Waserbia wenzake hao.
“Jerry Tegete analala chumba kimoja na Mrisho Ngasa kwa sababu wote wametoka Mwanza na wamecheza pamoja tokea utotoni, Godfrey Bonny analala pamoja na Nsajigwa kwa vile wote wanatoka Mbeya, Boniphace Ambani anakuwa na Ben Mwalala kwa kuwa wote ni Wakenya, hivyo hivyo kwa Abdi Kassim na Cannavaro (Nadir Haroub) kwa vile wanatokea Zanzibar.
“Kuna ubaya gani kwa Obren kuwa karibu na Kondic? Yeye hana mchezaji anayetoka naye Serbia,” alisema kuhusu tuhuma za Kondic kutokomea na Curkovic siku moja kabla ya kucheza Al Ahly hadi usiku wa manane.
Madega alikanusha kwamba Kondic na Curkovic walitokomea hadi usiku wa manane. “Tulichotakiwa kufanya ni kuwaacha wachezaji na benchi la ufundi katika hoteli moja na kisha watu wengine wangefikia sehemu nyingine, kitu ambacho kisingeleta maneno kama ya sasa,” alisema Madega.
Aidha, Madega alisema hata wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara kabla ya kumalizika ligi hiyo, hawatafanya sherehe zozote hadi warudiane na Al Ahly Aprili 4, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Latifa amtuliza Mrisho Ngassa
KIMWANA Latifa Abdul, ndiye mke mtarajiwa wa winga machachari wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mrisho Khalfan Ngassa, imeelezwa.
Kiungo huyo wa pembeni ambaye wakati mwingine huchezeshwa kama mshambuliaji, aliiambia DIMBA mwishoni mwa wiki kwamba, atafunga pingu za maisha na Latifa Mei mwaka huu.
“Mke wangu mtarajiwa anaitwa Latifa, tutafunga naye ndoa Mei, mwaka huu,” alisema Ngassa.
Kiungo huyo anatarajiwa kuondoka nchini Aprili 13, mwaka huu kwenda Uingereza kufanya majaribio katika klabu ya West Ham United, iliyovutiwa na kipaji chake.
Ngassa ambaye atakuwa huko kwa wiki mbili, akifuzu atakuwa mchezaji wa pili kutoka Afrika kujiunga na timu hiyo, baada ya beki wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Herita Nkolongo Ilunga.
Ngassa amepatiwa nafasi hiyo na wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) Yussuf Bakhresa, ambaye ndiye pia alimpatia nafasi ya kwanza, Januari mwaka huu nchini Norway, alipokuwa anatakiwa na klabu ya Lov Ham ya huko. Lakini uongozi wa Yanga uligoma kumruhusu.
Ngassa amezidi kuwa lulu baada ya kung’ara kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) iliyofanyika Ivory Coast mwezi uliopita, kiasi cha kuwavutia mawakala na wachambuzi mbalimbali wa mchezo wa soka.
“From my opinion, this young man is man of the match.” Hayo yalikuwa maneno ya mchambuzi na mtangazaji kwenye mchezo wa kwanza wa CHAN ambao Stars ilifungwa bao 1-0 na Senegal, akimaanisha: “Kwa maono yangu, huyu bwana mdogo ndiye nyota wa mchezo”.
Kinda la JKT lakaribia kumkamata Ambani
HUSSEIN Bunu, mshambuliaji chipukizi wa JKT Ruvu ya Pwani, anaweza kumpiku mkongwe Boniphace Ambani katika mbio za kuwania taji la ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iwapo atatumia vizuri mechi za mwishoni za Ligi hiyo.
Kwa sasa Bunu ana mabao 10, akizidiwa manne tu na Ambani, ambaye kasi yake ya kufunga imeonekana kupungua mzunguko wa pili wa Ligi hii akiwa amefunga bao moja tu katika mechi nne.
Bunu aliibukia kwenye Copa Coca Cola ya mwaka jana na alikuwamo kwenye kikosi cha vijana kilichokwenda mafunzoni Brazil ambako pia walishiriki mashindano na kubeba Kombe, ambalo walikwenda kulionyesha Bungeni mjini Dodoma.
Kinda huyo ambaye baadaye kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo alianza kumuita kwenye kikosi chake kwa ajili ya komkomaza, alisajiliwa na JKT Ruvu msimu huu na sasa ameibuka mfungaji tegemeo wa timu hiyo inayonolewa na Charles Killinda.
Wachezaji wengine ambao wanaweza kufanya maajabu na kumpiku Ambani ni Said Dilunga wa Toto Afrika ya Mwanza, mwenye mabao nane, Mussa Mgosi wa Simba mwenye saba, Ben Mwalala wa Yanga mwenye sita sawa na Orji Obinna wa Simba pia.
Nicolaus Kabipe wa Polisi Moro ana mabao matano sawa na Suleiman Kibuta wa Moro United, wakati Thomas Maurice wa Moro United ana mabao manne sawa na Paul Ngalioma wa Kagera Sugar, Philip Alando wa Azam, Bakari Kondo wa JKT Ruvu, Omar Matuta, Abdallah Juma wote wa Mtibwa Sugar, Idd Moshi wa Villa Squad na
Bantu Nsungwe wa Polisi Dodoma.
Villa yaweka rekodi ya kupigwa ‘Hat-trick’
TANGU msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza, wachezaji walioweza kufunga mabao matatu kwenye mechi moja ni watatu tu, Boniphace Ambani, Thomas Maurice na Hussein Bunu na wote walifunga kwenye mechi dhidi ya Villa Squad ya Kinondoni.
Villa, inayochungulia mlango wa kurejea Ligi Daraja la Kwanza, ilipigwa ‘Hat-trick’ ya kwanza Septemba 21, mwaka jana na Mkenya, Ambani katika mechi dhidi ya Yanga, iliyoibuka na ushindi wa 5-0.
Mabao mengine mawili ya Yanga siku hiyo yalitiwa kimiani na Ben Mwalala na Shamte Ally. Oktoba 17, Villa ilipigwa ‘Hat-trick’ ya pili na Maurice, aliyeiongoza Moro United kushinda 4-0, bao lingine likitiwa kimiani na Haji Dudu.
Machi 13, mwaka huu ilikuwa zamu ya kinda lililoibukia kwenye michuano ya kwanza ya Copa Coca Cola, Bunu ambaye alitikisa nyavu za Villa mara nne peke yake, timu yake JKT Ruvu ikiibuka na ushindi wa 5-1.
Bao jingine la JKT lilifungwa na Haruna Adolf, wakati la kufutia machozi la Villa, lilifungwa na mkongwe Iddi Moshi Shaaban.
Simba wote kuhamia Yanga J’mosi
MASHABIKI wa Simba, Jumamosi wiki hii watalazimika kuwashangilia wapinzani wao wa jadi, Yanga, wakati watakapokuwa wakimenyana na Kagera Sugar ya Bukoba kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
Kwa nini Simba wataishangilia Yanga siku hiyo? Kweli Yanga ni wapinzani wa jadi wa Simba, lakini siku hiyo Kagera ndio watakuwa wabaya wakubwa wa Wekundu wa Msimbazi, katika vita yao ya kuwania nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba inawania nafasi ya pili pamoja na Kagera Sugar, baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa kutokana na Yanga kujikusanyia pointi kibao hadi sasa, ambazo wao hawawezi tena kuzifikia.
Sasa Simba ambayo kunako majaaliwa isipoteleza tena kwenye mechi zake zilizosalia kwa kushinda zote, itafikisha pointi 42, inaomba Kagera ifungwe na Yanga ili ipunguzwe kasi katika vita yao ya kuwania nafasi ya pili.
Kagera, kabla ya kumenyana na Prisons mjini Mbeya jana, tayari ilikuwa ina pointi 27 baada ya kucheza mechi 16 wakati Simba yenye pointi sawa na hizo ilikuwa ina mchezo mmoja zaidi.
Pamoja na Simba kulazimika kwenda Uwanja wa Uhuru kuishangilia Yanga Jumamosi, Jumapili nao watakuwa na ngoma yao wenyewe, watakuwa wakimenyana na Azam FC ambayo kwa kipindi hiki haitaki ‘masihara’, kwani inahitaji kukusanya pointi za kutosha kujijengea kujiamini kwamba haitashuka.
Azam yaongoza kwa ‘Fair Play’ Ligi Kuu
KLABU ya Azam ndiyo angalau kitakwimu inaongoza kucheza soka ya kiungwana uwanjani (Fair Play), kutokana na kuwa timu yenye idadi ndogo zaidi ya kadi, 23 kati ya hizo zote zikiwa ni njano na nyekundu moja tu.
Yanga ndiyo inafuatia kwa mchezo wa kiungwana, kwani katika mechi 16 ilizocheza, imejikuta wachezaji wake wakipewa kadi za njano mara 24 na nyekundu mara mbili, wakati Simba imepewa kadi za njano mara 29 na nyekundu tano.
Kagera Sugar ina njano 25 na nyekundu mbili, Mtibwa Sugar njano 31 na nyekundu tatu, JKT njano 25, nyekundu mbili, Toto Afrika ina njano 32, nyekundu moja, Prisons njano 31, nyekundu moja, Polisi Morogoro njano 32, nyekundu tatu, Moro United njano 27, nyekundu mbili, Villa Squad njano 32, nyekundu mbili na Polisi Dodoma ina njano 30 na nyekundu nne.
Jumla ya kadi 340 za njano hadi sasa zimekwishatolewa kwenye Ligi Kuu, wakati nyekundu ni 28.
0 comments:
Post a Comment