// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); Thuwein: Mfungaji wa mabao ya Stars Lagos 1980 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE Thuwein: Mfungaji wa mabao ya Stars Lagos 1980 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Friday, February 06, 2009

    Thuwein: Mfungaji wa mabao ya Stars Lagos 1980


    NA MAHMOUD ZUBEIRY
    JE wamkumbuka Thuwein Ally Waziri(PICHANI JUU), mshambuliaji wa zamani wa klabu ya soka ya Simba ya Dar es Salaam na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars?
    Habari kuhusu wakali wengine wa soka wa zamani nchini kama Peter Tino, Zamoyoni Mogella, Jellah Mtagwa zimekuwa zikiandikwa na magazeti mbalimbali nchini, lakini vipi kuhusu Thuwein Ally Waziri, yuko wapi kwa sasa na anafanya nini?
    Thuwein Ally Waziri, mshambuliaji aliyekuwa maarufu kwa wanasoka wenzake kwa jina la utani kama 'Guu la Kushoto', kutokana na kutumia kwake mguu wa kushoto enzi zake, kwa sasa amestaafu soka na anaishi mjini Suwaiq, Oman.
    "Nipo, nimekwishakuwa raia wa huku tena, ninaishi sawa na Waarabu, naendana na mila na desturi zao, nimejifunza na kujua ninapaswa kuishi vipi, nashukuru maisha yangu yanaendelea vizuri tu,".
    Ndivyo alivyoanza kuzungumza Thuwein Ally bin Waziri katika mahojiano na bongostaz yaliyofanyika kwa njia ya simu, kutoka mji wa Thuwaiq anakoishi kwa sasa.
    Thuwein ni kati ya wachezaji bora waliowahi kutokea Tanzania, ambaye alikuwa akikonga nyoyo za mashabiki kwa jinsi alivyokuwa akiburuza kandanda kwa guu lake la kushoto.
    Ni guu lake hilo la kushoto lililokuwa likiwapiga chenga za maudhi mabeki mahiri na kuwatungua mabao matamu makipa hodari, enzi zake akicheza soka nchini.
    Mashabiki wanaposema siku hizi hakuna wachezaji Tanzania, wanakuwa wana hoja, kwa sababu wanakumbuka vyema wakali kama Thuwein waliifanyia nini nchi yao enzi zao.

    THUWEIN MFUNGAJI BORA WA STARS NIGERIA 1980:
    Sahau kuhusu Peter Tino aliyefungia Stars bao muhimu katika mechi dhidi ya Zambia mjini Ndola, mwaka 1979 na kufanya sare ya 1-1, hivyo kuipa Tanzania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Nigeria mwaka 1980.
    Sahau kuhusu Mohamed Adolph Rishard aliyefungia Stars bao pekee katika mchezo wa kwanza dhidi ya Zambia mjini Dar es Salaam, hivyo kwa matokeo ya 1-1 kwenye mechi ya marudiano mjini Lusaka, Tanzania ikajikatia tiketi ya kwenda Nigeria mwaka 1980.
    Sahau kuhusu Juma Mkambi aliyefunga bao la kufutia machozi wakati Stars inachapwa 3-1 Machi 8, mwaka 1980 na wenyeji Nigeria kwenye mechi ya ufunguzi wa fainali za Nigeria iliyokuwa ya Kundi A kwenye fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika.
    Thuwein Ally Waziri aliifungia Stars mabao yote matatu kwenye fainali za Nigeria, moja la kufutia machozi kwenye mechi dhidi ya wenyeji, Nigeria, lingine dhidi ya Misri na lingine la kusawazisha katika mchezo dhidi ya Ivory Coast.
    Tanzania ilipangwa kwenye kundi la kifo, A lililokuwa likitumia Uwanja wa Surulele mjini Lagos, dhidi ya wenyeji, Nigeria, Misri zilizofuzu kuingia raundi ya pili na Ivory Coast ambayo kama Stars ilifungashiwa virago baada ya mechi za kundi hilo.
    Machi 8, mwaka 1980 kwenye Uwanja wa Surulele, Thuwein alifunga bao lake dakika ya 54 na kufanya Nigeria iwe mbele kwa 2-1 badala ya kuongoza kwa 2-0 tangu dakika ya 35, Oyendika alipofunga bao la pili kufuatia Lawal kufunga la kwanza dakika ya 11, lakini Odegbami alishindilia msumari wa moto kwenye jeneza la Stars dakika ya 85.
    Machi 12, mwaka 1980 Thuwein Ally Waziri aliifungia Stars bao katika dakika ya 86, likiwa ni la kusawazisha baada ya Hassan Shehata, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Misri, kuwafungia Mafarao hao bao dakika ya 32 na Mosaad Nour dakika ya 38.
    Thuwein Ally Waziri tena Machi 15, 1980 katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo wa Stars, aliifungia timu hiyo bao dakika ya 59, kufuatia Kobenan kuifungia Ivory bao la mapema dakika ya saba.

    MAANDALIZI YA STARS HAYAKUWA MAZURI NIGERIA1980:
    Kwa mabao hayo, jina la Thuwein Ally Waziri limekuwa miongoni mwa majina makubwa na ambayo hayatasahaulika katika soka ya Tanzania.
    Akizungumzia mashindano hayo ya Nigeria, Thuwein anasema kwamba Stars ilikwenda huko bila ya maandalizi ya kutosha, licha ya ziara ya mafunzo nchini Mexico.
    "Kule timu zilikuwa zimeandaliwa zaidi kuliko sisi, japokuwa tulikwenda kule Mexico kwa maandalizi kabla ya mashindano kuanza, lakini tulionekana kama bado kiwango chetu kiko chini.
    Kwani tulitumia muda mwingi kuwasoma wenzetu kabla ya kuanza kucheza soka, na zaidi tulikuwa tukiibuka na kucheza vizuri kipindi cha pili na hata magazeti ya Nigeria yalikuwa yanaandika hivyo," anasema.
    Ingawa alikwenda Nigeria na Stars kama mshambuliaji wa Simba, lakini kisoka Thuwein Ally Waziri aliibukia visiwani Zanzibar, alikozaliwa na kukulia.

    THUWEIN ALIVYOWAPIGA 'HAT-TRICK' MUFULIRA 1979:
    Kwani nini mashabiki wa Simba hawatamsahau Thuwein Ally Waziri? Ni kutokana na upara wake ulioanzia juu ya paji la uso kuelekea nyuma ya kichwa chake au kwa uchezaji wake wa kutumia guu la kushoto?
    Inawezekana hayo yakachangia, lakini kikubwa ni vitu vyake alivyofanya nchini Zambia mwaka 1979, Simba ilipokuwa ikirudiana na Mufurila Wanderers katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, sasa Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Simba ilikwenda Zambia ikiwa mashabiki wake wamekwishakata tamaa ya kusonga mbele, baada ya kipigo cha nyumbani cha mabao 4-0 ilichokipata kutoka kwa Wazambia hao mjini Dar es Salaam.
    Lakini katika hali iliyowastaajabisha wengi, kwenye mchezo wa marudiano Wekundu wa Msimbazi, waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 mjini Lusaka, matatau yakifungwa na Thuwein Ally Waziri, mawili na George 'Best' Kulagwa.
    "Kwa kweli mchezo ule kuna vitu viwili au vitatu vilitufanya tushinde, kikubwa ni kwamba wachezaji wenyewe tulisema kwamba, kama hawa wametufunga 4-0 nyumbani, na sisi tutakwenda kuwafunga kwao zaidi ya walivyotufunga.
    Na kweli, tulipofika kule pamoja na kuzomewa na Wazambia, walikuwa wakitutambia sisi tumekwenda kufungwa mabao mengine sita na kila aina ya kejeli, lakini sisi tulikuwa na dhamira moja tu, kucheza kwa bidii ili tushinde.
    Tulipeana majukumu, kila mtu acheze kwa juhudi, mabeki wasiruhusu magoli na kule mbele tutafute mabao kwa jitihada kubwa na tukafanikiwa, nakumbuka mimi peke yangu nilifunga magoli matatu safi, mengine alifunga George Kulagwa kama sikosei (mawili),"anakumbuka Thuwein.
    Kwa matokeo hayo, Simba ilifuzu kuingia Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na Racca Rovers ya Nigeria.
    Mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana 0-0 na ziliporudiana mjini Lagos, Rovers walishinda 2-0, hivyo Simba kutolewa.

    THUWEIN ALLY WAZIRI, MWANA ZANZIBAR:
    Mpachika mabao huyo nyota wa zamani nchini Tanzania, alizaliwa Aprili 6, mwaka 1959 visiwani Zanzibar na alipata elimu yake ya Msingi katika Shule ya Darajani, kabla ya kujiunga na sekondari ya Haille Selassie visiwani hivyo maarufu kwa zao la Karafuu.
    Mbali na kucheza soka shuleni, Thuwein pia alichezea timu za watoto za Everton na Small Simba kabla ya kusajiliwa na klabu bingwa ya zamani Tanzania, Malindi iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar, sasa Ligi Kuu mwaka 1975.
    Aliichezea Malindi hadi mwaka 1979 alipohamia kwenye klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, ambako alicheza hadi mwaka 1982 na kutimkia Kenya kujiunga na klabu ya Belham, iliyokuwa Daraja la Pili kwa muda wa miezi mitatu.

    THUWEIN ALLY WAZIRI, KOPLO WA JESHI LA ABU DHABI:
    Kutoka hapo, Thuwein alikwenda moja kwa moja Abu Dhabi, Falme za Kiarabu kuchezea timu ya jeshi la nchi hiyo hadi mwaka 1987 alipohamia Al Suwaiq ya Oman, ambayo aliichezea hadi mwaka 2002, alipoamua kutundika daluga zake.
    Alipofika Abu Dhabi, Thuwein anasema kwamba alipata mafunzo ya kijeshi na kuajiriwa na jeshi la Abu Dhabi, alilolitumikia hadi mwaka 1992 na kustaafu.
    "Niliishia kwenye cheo cha koplo tu, unajua tena mambo ya jeshi, sisi zaidi tulikuwa kwenye soka tu, kwa hivyo mambo mengi ya kijeshi tulikuwa hatushiriki sana,"anasema Thuwein.
    Ingawa alikuwa mshambuliaji hodari nchini Tanzania, lakini baadaye Thuwein alipokwenda Uarabuni alihamia kwenye safu ya kiungo na mwishoni akawa beki na hadi anastaafu alikuwa mlinzi hodari wa klabu yake Al Suwaiq.
    Baada ya kustaafu, Thuwein anasema kwamba sasa kwa uzoefu wake amekuwa mmoja wa wataalamu wa benchi la ufundi la klabu yake kipenzi, iliyo katika mjini anaoishi, Al Suwaiq.

    THUWEIN ALLY WAZIRI, MFANYAKAZI WA HOTELI SUWAIQ:
    Kwa sasa Thuwein Ally Waziri anafanya kazi katika hoteli kubwa na maarufu nchini Oman, Al Suwaiq ya mjini Suwaiq.
    "Katika hii hoteli mimi kazi yangu ni kusimamia wasaidizi wa wageni wanaofika hapa, hayo ndiyo majukumu yangu ya kila siku,"anasema.
    Al Suwaiq ni mji uliopo pwani ya mkoa wa Al Baţinah, Kaskazini Mashariki mwa Oman na hilo ni neno la Kiarabu ambalo, Kiswahili tafsiri yake ni Soko.
    Mji huo ulipachikwa jina hilo kwa sababu uko katikati ya mkoa wa AL Batinah, hukusanya idadi kubwa ya watu wanaoishi milimani pamoja na watu wanaoishi maeneo ya pwani, ambao huenda kuununua na kuuza bidhaa mbalimbali.
    Thuwein alichaguliwa kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya Tanzania Juni, mwaka 1979 akiwa anachezea klabu ya Simba.
    Miongoni mwa mechi za awali kuichezea timu hiyo ya taifa ambazo anasema hatazisahau daima maishani mwake, ilikuwa dhidi ya Kenya, Harambee Stars, ambayo aliiwezesha Stars kuibuka na ushindi wa mabao 5-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ingawa hajasoma kozi yoyote ya ukocha, lakini Thuwein anasema kwa kutumia uzoefu tu yeye ni kocha bora, ambaye anaweza kufundisha timu yoyote kubwa barani Afrika.
    "Lakini sijawahi kufundisha timu yoyote, zaidi ya timu yangu tu, Suwaiq, ila kwa jinsi ninavyojijua mwenyewe, nina imani timu yoyote nikipewa naweza kufundisha na ikafanya vizuri,"anasema.

    KWA NINI HATAKI KUFUNDISHA TIMU, WAKATI NI KOCHA MZURI?
    "Ukocha unataka uvumilivu mkubwa na uwe makini katika maamuzi yako na kujua kuishi vizuri na wachezaji wako, pia uwe mzuri wa kuzisoma timu pinzani wakati wa mchezo,"anasema.
    Thuwein anasema si kama yote hayo hayawezi, bali hataki kujikita kwenye soka moja kwa moja kwa sababu ya kupata muda wa kutosha wa kuwa karibu na familia yake.
    "Nimecheza soka takriban miaka 33, muda wote zaidi nilikuwa nazitumikia klabu na timu za taifa, sikupata muda wa kutosha kuwa na familia yangu hata nao wakajisikia haswa wako na mimi.
    Sasa tangu nimestaafu soka, napenda kazi zangu za kila siku pale Al Suwaiq Hotel, niwe na familia yangu, soka sasa nimemuachia mwanangu, naamini yeye ataliendeleza jina langu,"anasema.

    THUWEIN ALLY WAZIRI APATA MRITHI WA GUU LA KUSHOTO:
    Thuwein ni mume wa Habiba Rashid, ambaye amebahatika kuzaa naye watoto watatu, wawili wa kike ambao ni Khadija na Moza, mmoja wa kiume, aitwaye Abdul Hadi ambaye anafuata nyayo zake kwenye soka.
    "Mtoto wangu anacheza mpira katika timu za watoto, kwani bado anasoma, vile vile anatumia mguu wa kushoto kama mimi baba yake, naamini atakuja kuwa mchezaji mkubwa baadaye,"anasema Thuwein.
    Thuwein anasema ingawa mwanawe ni raia wa Uarabuni, lakini atapenda siku moja naye akachezea klabu ya Simba ya Dar es Salaam, ambayo aliichezea baba yake.
    "Hakuna kisichowezekana bwana, huyu mimi ninakuambnia ni mchezaji mzuri, ninachokifanya kwa sasa ni kumuendeleza tu, Simba wamsubiri tu, siku moja atakuja kuwafanyia mambo huko,"anasema.

    THUWEIN ANAFAHAMU LOLOTE KUHUSU SOKA YA TANZANIA?
    Thuwein anasema kwamba bado anafuatilia soka ya Tanzania kwa kusoma kwenye mitandao, hivyo anafahamu kinachoendelea nchini.
    "Ila kwanza napenda kuzungumzia kuhusu timu ya taifa, wamefanya jambo la maana kupata kocha wa kigeni, tena kutoka nchi kama Brazil yenye kujua soka haswa. Mafanikio yatakuja tu, Watanzania wawe wavumilivu.
    Kwa sasa jambo la msingi ni kumpa ushirikiano huyo kocha na pia viongozi wa soka wahakikishe maandalizi yanakuwa mazuri zaidi, mechi za majaribio ziwe nyingi.
    Pili, nawageukia wachezaji wa Tanzania, naomba sana waache ubinafsi katika timu ya taifa, waondoe itikadi za wewe Simba, mimi Yanga, huyu Mzanzibari, wacheze kwa moyo,"anasema.

    KWA THUWEIN ALLY WAZIRI, LIGI NDEFU YA KAZI GANI?
    Akizungumzia Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, inayodhaminiwa na Kampuni za Vodacom na GTV, Thuwein anasema kwamba hakuna sababu ya kufanywa kuwa ndefu, inapaswa kuwa fupi ili kuzipa nafasi programu nyingine za maendeleo.
    "Ligi isifanywe ndefu, kutokana na hali ilivyo pia itafanya wachezaji kuchoka, iwe fupi lakini nzuri, vile vile timu zipate makocha wazuri, ndiyo ligi itapokuwa nzuri zaidi na klabu zitatoa wachezaji wazuri katika timu ya taifa,"anashauri.
    Thuwein anampongeza kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo kwa kazi yake nzuri aliyoifanya hadi sasa, kwani soka ya Tanzania imepiga hatua kwa kipindi cha mwaka mmoja tu wa kuwapo kwake nchini na Mbrazil mwenzake, Msaidizi wake, Itamar Amorin.

    ANASEMAJE KUHUSU KLABU YAKE YA ZAMANI SIMBA?
    Akiwa mchezaji aliyecheza kwa mafanikio Simba kabla ya kuikacha klabu hiyo, Thuwein hajasahau moja kwa moja kuhusu timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
    "Ushauri wangu kwa mashabiki wa Simba, la muhimu kwao na lililo kubwa ni kuacha tabia ya kutoa maneno machafu kwa mchezaji wakati anapokosea kutoa pasi vizuri au kukosa kufunga goli.
    Kumtolea maneno machafu mchezaji ni kumvunja moyo, lazima wamshangilie hata pale anapokosea, na wawe na moyo wa kimichezo pale timu inaposhindwa na timu nyingine, wawe wavumilivu, hiyo ndiyo soka,"anasema.

    KIKOSI GANI KIKALI ZAIDI CHA STARS ANACHOKIKUMBUKA?
    Thuwein anasema amecheza timu ya taifa tangu mwaka 1979 hadi 1982 alipotimkia Uarabuni, lakini kikosi anachokikumbuka zaidi ni kile cha mwaka 1981 na 1982.
    Anasema ndani ya kikosi hicho kulikuwa kuna wakali kama Juma Pondamali, Mussa Kihwelo, Ahmed Amasha, Leodegar Tenga, Salim Amiri, Jella Mtagwa, Mohamed Adolf Rishard, Hussein Ngulungu, yeye mwenyewe,
    Muhammed Salum, Omar Hussein, Juma Mkambi, Leopold Mukebezi, Peter Tino, chini ya kocha Joel Bendera.
    Naam, huyo ndiye Thuwein Ally Waziri, nyota aliyeifungia Simba mabao matatu wakati ikishinda 5-0 mjini Lusaka, Zambia dhidi ya wenyeji, Mufurila Wanderers katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, na kuilipa kisasi cha kuchapwa 4-0 nyumbani, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: Thuwein: Mfungaji wa mabao ya Stars Lagos 1980 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top