Manji akifurahia kwa raha zake na rais wa zamani wa Yanga, Francis Mponjoli Kifukwe
na saleh ally
HUKU kukiwa na uvumi wa kutaka kujiondoa kwa mfadhili mkuu wa Yanga, miezi michache ijayo, bilionea huyo ametoa ofa nyingine kwa wana Jangwani kwa kuongeza ghorofa zaidi katika upande moja wa makao makuu wa Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam. Habari za uhakika ambazo imezipata Mwanaspoti ni kwamba, Manji amekubali mabadiliko ya ukarabati baada ya kampuni inayoshughulikia ujenzi katika makao makuu ya Yanga eneo la Jangwani kuamua kubadili ramani ambayo itaongeza gharama. Manji amekubali kutoa kitita kingine kwa ajili ya ujenzi huo baada ya ramani mpya kuonyesha kwamba inalazimika kuongezwa upande mmoja wa ghorofa na pia sehemu ya maegesho ya magari kwa ajili ya wageni na wachezaji. "Lakini pia, ramani inaonyesha lazima kuwe na 'gym' ambayo katika ramani ya mwanzo haikuwepo. Gharama imeongezeka kwa kiasi kikubwa lakini Manji amekubali kugharimia," kilieleza chanzo hicho. Imeelezwa bado majadiliano ya kitaalamu yanaendelea kuhusu suala la Uwanja wa Kaunda kuwekewa nyasi bandia au za kawaida. "Bado halina uhakika kwa kuwa kitaalamu inaonyesha kama wataweka nyasi bandia wachezaji watakuwa wanacheza mechi nyingi katika nyasi za kawaida ukiachana na Uwanja wa Taifa. Sasa walikuwa wanaangalia waweke nyasi bandia au waweke za kawaida. Wengine walisema matunzo ya nyasi za kawaida ni makubwa na yanahitaji uangalizi makini. "Kwa hiyo bado wanajaribu kuwasiliana na wataalamu mbalimbali ili kujua nini kifanyike kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho wa suala hilo wakati ukarabati mwingine ukiendelea," kilieleza chanzo. Mwanaspoti ilifanikiwa kumpata Manji juzi Alhamisi, ambaye alisema kwa ufupi kuhusu suala hilo; "Ukarabati unaendelea na kuna mambo kadhaa yamebadilika, nafikiri tuwaachie wataalamu wafanye kazi." Alipoulizwa suala lake kuamua kutoidhamini Yanga alisema; "Nani kasema, nafikiri utaona ujenzi unaendelea na mambo mengine zaidi." Hata hivyo, chanzo kingine kilieleza kwamba, Manji huenda akaachana na Yanga baada ya kukamilisha kila kitu kama alivyoahidi. "Angalia, itakuwa ni hosteli ya kimataifa ambayo sidhani kama kuna klabu ya Afrika Mashariki na Kati inamiliki. Baada ya hapo, nafikiri ataendelea na mambo mengine na kuiacha Yanga ambayo siku zote amekuwa akisistiza ijitegemee,"kilieleza chanzo hicho cha uhakika. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kutaka kuondoka kwa Manji kuendelea kuidhamini Yanga, ingawa Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega alisema kwamba mfadhili huyo bado yuko bega kwa bega na klabu hiyo kongwe.
0 comments:
Post a Comment