RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapata fedha nyingi zaidi za viingilio kuliko timu husika na kulitaka litumie fedha hizo kuiendesha timu ya taifa, Taifa Stars.
Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana wakati wa chakula cha mchana alichowaandalia wachezaji wa Stars, Kikwete alisema kuwa TFF ndiyo yenye jukumu la kuiendesha Stars, wakati yeye akimlipa kocha wa timu hiyo.
TFF ndiyo inayosimamia mapato ya viingilio vya uwanjani vya mechi za Stars, lakini katika mechi zinazochezwa katika Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam, inafanya hivyo kwa ushirikiano na Kamati Maalum iliyoundwa na Serikali inayosimamia uwanja huo.
Mbali na mechi za Stars, hata zile za klabu zilizopo chini yake (za Ligi Kuu na za kimataifa), TFF huwa inapata mgao wa fedha za viingilio.
ÒNimesikia mnapata fedha nyingi zaidi za viingilio kuliko timu, viingilio vya mlangoni chukueni lakini visaidie timu ya taifa,Ó alisema.
Rais aliwashukuru wadhamini wa Stars kutokana na jinsi wanavyoisaidia timu hiyo na hatimaye kufikia hatua iliyopo sasa kwa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Ivory Coast.
Akizungumzia juu ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN), Rais Kikwete aliwataka wachezaji wa Stars wahakikishe wanacheza kadri ya uwezo wao ili wafanye vizuri.
ÒMnaposhinda Watanzania hawapati usingizi, wanakesha wakishangilia kwa furaha, lakini mkishindwa, wanakuwa wanyonge. Hata mimi ninakuwa mnyonge sana mnaposhindwa,Ó alisema.
Stars leo inatarajiwa kushuka katika uwanja wa zamani wa Taifa kuumana na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, ukiwa ni maalum kwa maandalizi ya fainali za CHAN ambazo timu zote hizo zitashiriki.
Rais Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwataka wachezaji hao kushinda mechi ya leo ili kutuma salamu kwa timu pinzani katika CHAN.
0 comments:
Post a Comment