na abdul mohammed, abidjan
KITENDO cha timu ya Taifa ya Tanzania kuwalaza wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) bila shaka kimepokelewa kwa mashangao mkubwa.
Mshangao huo unatokana na fikra kwamba soka ya Afrika Magharibi iko juu na kwamba ni vigumu kwa timu za Afrika Magharibi kufungwa na timu za Afrika Mashariki hususan Tanzania.
Bila shaka hapa watahusishwa wachezaji kadhaa mahiri wa Ulaya katika kuthibitisha kwamba Stars kamwe haingeweza kuibuka na ushindi .
Watatajwa kina Didier Drogba, Kolo Toure, Yaya Toure, Solomon Kalou na wengineo kuthibitisha ubora wa timu hizo na kwamba haingekuwa jambo rahisi kwa Stars kuibuka na ushindi katika nchi ambayo mastaa hao wa Ulaya wanatokea.
Kwa maana nyingine umahiri, umakini na ubora unaofanana japo kwa mbali na ule wa kina Kolo na Drogba ndio ambao Stars wangekutana nao.
Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kwani hatimaye walikuwa ni Stars walioibuka na ushindi kwa bao safi lililofungwa na Mrisho Ngassa aliyeunganisha krosi ya Henry Joseph
Ndani ya uwanja:
Bao hilo ni sehemu tu ya juhudi za wachezaji wa Stars katika kuupata ushindi huo wa kujivunia, Wachezaji wa Stars kuanzia mabeki hadi washambuliaji walionekana kubadilika ukilinganisha na hali ilivyokuwa katika mechi ya kwanza dhidi ya Senegal.
Kuanzia kwa mabeki, uhai wa Nsajigwa uliongezeka kwa upande wa kulia, Juma Jabu ambay e ni beki wa kushoto licha ya kuathiriwa na tatizo la ufupi lakini alionekana kuwa makini kwa wakati wote licha ya makosa ya hapa na pale yaliyokuwa yakijitokeza upande wake.
Ukija kwa mabeki wa kati umakini wao ulidhihirika uwanjani, hata kwa wachambuzi na waandishi wengine wa nchi mbalimbali walisifu ushirikiano wa Salum Sued na Nadir Haroub Cannavaro.
Wakati wa mapumziko nilipata bahati ya kukutana na Mkurugenzi wa ufundi wa timu ya Senegal, Barnour Ell na kumuomba anipe tathmini fupi ya mchezo, alianza kwa kuisifia Tanzania na kuiponda Ivory Coast lakini zaidi alisema walinzi wa kati wametulia.
Ni wazi kwamba umakini wa mabeki hao ulikuwa kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa Ivory Coast kuipasua ngome ya Tanzania.
Kipa Shaaban Dihile naye bila shaka kazi yake golini ilirahisishwa na safu ya ulinzi ya Tanzania ingawa naye alionyesha uhai wakati fulani katika kukabiliana na washambuliaji wa Ivory Coast.
Umakini wa safu hiyo na kipa wao Dihile bila shaka unadhihirishwa na namna ambavyo walizidhibiti kona 11 za Ivory Coast zilizoelekezwa katika lango la Stars.
Safu ya kati kidogo ilionekana kupwaya, Henry Joseph alikuwa na wakati mgumu kutawanya mipira na kuwadhibiti Ivory Coast na hilo bila shaka lilithibitishwa na kocha Marcio Maximo ambaye baadaye aliamua kumtoa na baada ya mechi alisema kwamba mchezaji huyo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo.
Kuna wakati kupwaya huko kwa Henry Joseph kulionekana kumpa wakati mgumu kidogo Nizar Khalfan.
Hata hivyo pamoja na hali hiyo lakini Henry Joseph wakati wote alikuwa mpiganaji, alipambana katika hali hiyo hiyo hadi kocha alipoamua kumtoa.
Nurdin Bakar naye pamoja na matatizo ya hapa na pale ambayo mengi ni ya kawaida lakini kiujumla alionyesha uhai, alionyesha umakini wa hali ya juu, aliwadhibiti vyema Ivory Coast na kuwaunganisha wachezaji wenzake.
Mchezaji mwingine ambaye alidhihirisha upiganaji wa uhakika alikuwa ni Mussa Hassan Mgosi, Mgosi ambaye katika mechi ya kwanza na Senegal aliingia kipindi cha pili alidhihirisha upiganaji, hakuwa mwenye kukata tamaa katika kutafuta mipira kwa kukaba badala ya kusubiri kupasiwa na hata kujaribu kulisogelea lango la Ivory Coast.
Kwa aliyemfuatilia Mgosi kwa makini anaweza kubaini kwamba alipania kufanya vitu vyake katika mechi ile.
Bila shaka kutokana na mchango mkubwa wa Mgosi katika mechi na Ivory Coast unaweza kupata hisia kwamba katika mechi na Senegal Maximo alipaswa kumchezesha Mgosi kuanzia mwanzo badala ya Tegete.
Kama ilikuwa ni lazima kumchezesha Tegete basi mchezaji huyo alifaa kuingia kipindi cha pili kama ambavyo Maximo alifanya katika mechi na Ivory Coast.
Hata hivyo ukimuuliza Maximo kuhusu hilo mbali na sababu za kiufundi anazoweza kukupa lakini siku zote anafahamika kwa kuwa mfuasi wa wachezaji chipukizi na wakati mwingine inakuwa vigumu kumbishia kwa kuwa matunda yake yanaonekana.
Mrisho Ngasa ambaye kwa waliomzoea watakiri kwamba alikuwa na wakati mgumu katika mechi na Senegal, alishindwa kuonyesha makeke ambayo wengi wamezoea kuyashuhudia anapokuwa na timu ya Taifa.
Katika mechi na Senegal kushindwa kufurukuta kwa Ngassa kunahusishwa na sababu tatu, kwanza ni Stars kucheza mipira ya juu ambayo ilikuwa ikimzidi kimo mchezaji huyo kutokana na ufupi wake, pili ni nafasi yake kwamba hakuwa nafasi ya pembeni kama ilivyozoeleka na hivyo kushindwa kukimbia na mipira na kupiga chenga.
Tatu kushindwa kutamba kwa Ngassa katika mechi na Senegal kunahusishwa moja kwa moja na mtu anayeitwa Ndiaye Sidy, beki wa Senegal ambaye alimbana Ngassa.
Sidy alipewa kadi ya njano katika dakika ya 19 kutokana na rafu mbaya aliyomchezea, Ngassa ambaye alikuwa tayari amemuacha.
Zaidi ya hilo mara kadhaa Ngassa alipewa pasi na Nurdin Bakar dakika ya 36, Nsajigwa dakika ya 34 lakini mguu wa Sidy ulimbana vilivyo na zaidi ya hilo mipira mingi ya juu Sidy aliweza kuitawala kiulaini na kumfunika Ngassa.
Mambo yalikuwa tofauti kwa Ngassa katika mechi na Ivory Coast, aliweza kukimbia na mipira mara kadhaa na wakati mwingine kupiga chenga na hata bao alilofunga lilidhihirisha umahiri wake, aliupigia hesabu nzuri mpira na kuurukia hadi kuujaza wavuni kwa kichwa (diving header).
Nje ya uwanja
Nje ya uwanja nako kulikuwa na mambo yake, kocha Maximo aliwaambia wachezaji wake kutumia udhaifu wa Ivory Coast ili kupata ushindi.
Aliwaambia Ivory Coast wana presha ya kufungwa na zaidi ya hilo presha yao ni zaidi kwa kuwa wamefungwa wakiwa nyumbani.
Katika hatua nyingine wachezaji wa Stars walilazimika kukwepa kula chakula cha asubuhi na mchana katika hoteli ya Golf waliyofikia.
Viongozi wa TFF badala yake walitoa nafasi kwa watanzania wakiwamo waandishi wa habari kula chakula cha asubuhi katika hoteli hiyo, hali ilikuwa hivyo hivyo kwa chakula cha mchana, wachezaji hao badala yake walikodiwa teksi ambazo ziliwapeleka kula chakula cha asubuhi na mchana sehemu nyingine.
Sambamba na hilo, wachezaji hao pia walikataa ofa ya kufuliwa jezi ambayo ilitolewa kabla ya mechi na wenyeji na zaidi ya hilo hata basi ambalo Stars walipewa kwa ajili ya kwenda uwanjani na sehemu nyinginezo nalo pia walilikataa na kukodi basi jingine badala yake basi hilo lilitumiwa na watanzania waliofika kuishuhudia Stars.
0 comments:
Post a Comment