// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); UBABAISHAJI WA VIONGOZI SIMBA, YANGA... - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE UBABAISHAJI WA VIONGOZI SIMBA, YANGA... - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Tuesday, January 20, 2009

    UBABAISHAJI WA VIONGOZI SIMBA, YANGA...


    KWA VIONGOZI HAWA, SIMBA YANGA HAZITAFIKA POPOTE!

    na mahmoud zubeiry
    NOVEMBA mwaka juzi Shirikisho la Soka la Kimataifa(FIFA) liliendesha semina kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu nchini, iliyofanyika Bagamoyo na kutoa mwongozo wa uendeshaji mchezo huo kisasa.
    Kubwa lilikuwa kutayarisha Katiba mpya ambazo zitabeba mfumo wa kuendesha klabu kisasa, ikizingatiwa mchezo huo hivi sasa ni zaidi ya mchezo, kwani mpira wa miguu hivi sasa ni biashara kubwa yenye maslahi makubwa pia.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliipa uzito mkubwa semina hiyo na kuziagiza klabu, ili zishiriki msimu huu wa Ligi Kuu zinapaswa kwanza kuwasilisha Katiba mpya kulingana na maelekezo ya azimio la Bagamoyo.
    Ilishuhudiwa klabu zikienda mbio dakika za lala salama kuitisha mikutano ya wanachama kuhakikisha zinapitisha rasimu zao, ili Katiba ziwasilishwe TFF na hatimaye kuepukana na hatari ya kuondolewa kwenye Ligi Kuu.
    Hakika zoezi hilo lilikuwa lenye ufanisi mkubwa, kwani klabu zote za Ligi Kuu ikiwemo zile zilizopanda msimu huu, zilitekeleza agizo hilo na hatimaye zipo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Tanzania Bara.
    Hata hivyo, inasikitisha kwamba Katiba hizo zilitengenezwa kama geresha tu, ili kuiridhisha TFF isiziengue timu katika Ligi Kuu, kwani hadi sasa utekelezaji wake bado haujafanyika.
    Kubwa linaloelekezwa kwenye rasimu hiyo ni klabu kuajiri sekretarieti, ambayo itafanya shughuli za kila siku za klabu, ikiwemo kupanga na kuratibu mipango ya maendeleo.
    Kwa mfano TFF ina sekretarieti yake chini ya Katibu Mkuu, Frederick Mwakalebela, ambayo ndio imekuwa ikifanya shughuli za kila siku za shirikisho hilo, kusimamia na kuratibu mipango ya maendeleo.
    Kamati ya Utendaji kama chombo cha juu na mwajiri wa sekretarieti imebaki na jukumu la kusimamia sera na kufuatilia utendaji wa sekretarieti yake, ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
    Naam, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, matunda ya sekretarieti ya TFF yameonekana, hapana shaka akina Mwakalebela wanafanya kazi, kwani imeshuhudiwa jinsi TFF ilivyojipambanua na kuwa asasi imara, kuliko kabla ya kuanza kwa mfumo huu.
    Ilikuwa imani ya wengi kwamba, baada ya klabu kuwasilisha Katiba mpya zinazoelekeza mfumo mpya na wa kisasa wa uendeshwaji wa klabu, kitakachofuata ni utekelezaji wake ambao pengine baada ya muda mfupi, ungeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, soka na taswira ya klabu zenyewe kwa ujumla.
    Katika hili klabu kongwe za Simba na Yanga zilitarajiwa kuwa mfano wa kuigwa, kwamba kwa sababu ya kuwa na wapenzi wengi, zingeweza kuifanyia kazi changamoto hiyo na kusubiri kuvuna matunda yake.
    Ilikuwa jambo la kufurahisha kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, klabu hizo za Dar es Salaam, zilipata mkataba wa udhamini, kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro.
    Katika Mkataba huo, TBL pia ilielekeza klabu hizo ziajiri sekretarieti mara moja, hicho kikiwa kipengele muhimu kwenye mkataba ambacho zilistitizwa kukitekeleza.
    Lakini siku zinayoyoma, si kwa azimio la Bagamoyo wala Mkataba wa TBL, viongozi wa Simba na Yanga wameweka nta kwenye masikio yao, hawataki kuajiri sekretarieti.
    Inasikitisha Mwenyekiti wa klabu moja kati ya hizo, alipoulizwa na Mwandishi wa Makala haya kuhusu suala hilo, alisema kwamba ni gharama kubwa kuajiri sekretaieti, hivyo klabu yake haiwezi.
    Huo ndio ulikuwa mtazamo wa kiongozi huyo, kwamba ni hasara kwa sababu ya kulipa mishahara ya watendaji hao, lakini hakufikiria ni faida gain itakayotokana na kuwapo kwa watu katika klabu yake.
    Inafahamika wazi viongozi wa klabu kama Yanga hawana muda wa kutosha kufanya kazi za klabu, bali hiyo ni kazi ya ziada baada ya shughuli zao za kila siku zinazowapatia riziki za kuishi na familia zao.
    Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega ambaye ni Wakili, saa ngapi atafanya kazi zake za Uwakili na saa ngapia atakaa ofisi ya klabu yake kufanya kazi za kila siku za klabu hiyo?
    Unakuta kwake hiyo ni kazi ya ziada, kwamba atafanya mambo ya Yanga baada ya kazi zake za kila siku, vivyo hivyo kwa Katibu Mkuu Lucas Kisasa, bosi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, anapaswa kuwa ofisini pale Lumumba kila siku, je shughuli za klabu atazifanya saa ngapi?
    Ni kwa sababu hiyo, Sekretarieti ni muhimu katika mfumo wa sasa, kwani Katibu Mkuu ndiye atakayeandaa mapendekezo ya miradi na masuala mbalimbali, ndiye atakayefuatilia mali za klabu na matunda yake.
    Ardhi ni rasilimali kubwa, Yanga imebahatika kuwa mmiliki wa ardhi katika maeneo ya mijini, inaelezwa mbali na Jengo la Jangwani, klabu hiyo ilikuwa ina nyumba Mtaa wa Mafia, Tandale na Buguruni, zote hizi nani anazifuatilia? Zinainufaisha vipi klabu hiyo?
    Mfano mzuri ni watani wao wa jadi, Simba, kizazi cha sasa Simba kilirithi jingo moja na eneo kidogo la wazi, lakini wakati Kassim Dewji akiwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, aliiwezesha klabu hiyo kujenga jingo la pili katika eneo la wazi.
    Lakini jambo la kustaajabisha unapohoji masuala kama haya, baadhi ya viongozi wanaibuka na hoja za kuhujumiwa kwa sababu timu zao zipo vizuri hivi sasa, huo uzuri uko wapi ikiwa klabu zao hazina dira wala mwelekeo?
    Viongozi wa klabu hizi waje na hoja za kujibu hoja, kwani nini wameshindwa kutekeleza azimio la Bagamoyo? Klabu kama Yanga kwa mfano, inapaswa kuonyesha tofauti yake na klabu nyingine kutoka na hali yao nzuri kiuchumi ukilinganisha na klabu nyingine.
    Yanga ina wafadhili wawili, Yussuf Manji aliyebeba majukumu makubwa zaidi ikiwemo kukarabati jengo la klabu hiyo na TBL, wakati watano wao jadi Simba wana mdhamini mmoja tu Kilimanjaro.
    Lazima ifike wakati klabu hizi ziondokane na hali ya utegemezi, ili wakati mwingine zisikubali hata kupewa mikataba isiyowanufaisha, kwa sababu tu hawana jinsi kutokana na hali yao ye utegemezi.
    Leo Simba na Yanga zikiweza kujimudu bila ya kutegemea mtu au asasi, zitakuwa na nafasi nzuri mno ya kuukubali au kuukataa udhamini usio na manufaa kwao. Lakini kwa sababu ya utegemezi wao, hawana jeuri ya kuukataa mkataba wa udhamini wa aina yoyote, hata wenye kuwakandamikza, kwa sababu wanachohitaji wao ni hizo fedha tu.
    Lakini kama kutakuwa na Sekretarieti sambamba na Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu, ndio watakaopanga na kusimamia mipango ya maendeleo ya klabu hizi, kuanzia ya muda mfupi, kati na mrefu.
    Hapana shaka mapato ya jezi, kofia, mifuko, stika, vitambaa vyote ambavyo wapenzi wa klabu hizi wananunua zikiwa na nembo ya klabu zao, zitaanza kuinufaisha klabu hizo moja kwa moja. Majengbo ya klabu hizo yataboreshwa na yatatumiwa kibishara yazinufaishe kjlabu zenyewe, kwa mfano Yanga yenye majengo mengi, hapana shaka itanufaika zaidi.
    Lakini hali ilivyo sasa, viongozi wa klabu hizi hawawezi kuongoza klabu hizo kwa ufanisi, pasipo kufuata maelekezo ya azimizo la Bagamoyo.
    Kama kweli klabu za Tanzania zinataka mafanikio ya kweli, hazina budi kuukubali muundo wa kisasa wa utawala, ambao hakika ndio ukombozi wa kuweza kuzifanya zifanane na klabu nyingine barani.
    Hoja kwamba Tanzania haifanani kiuchumia na nchi nyingine, hivyo haiwezi kufuata muundo wa kisasa wa uendeshwaji wa klabu ni mapungufu ya uelewa katika suala la uongozi.
    Kwani uchumi ni kitu ambacho kinatengenezewa misingi ya kukua kwake na mojawapo ni kuwa na watalaamu ndani ya klabu ambao watabuni miradi ya kuiongezea pato klabu.
    Kama Mkurugenzi wa Ufundi atatengeneza programu nzuri ya soka ya vijana na klabu ikaweza kuzalisha vipaji vya kuuza Ulaya, dhahiri klabu itanufaika na mradi huo.
    Aliyekuwa kocha wa Yanga kabla ya Kondic, Milutin Sredojevic ‘Micho’ akiwa na klabu hiyo nchini Tunisia mwaka 2006, alivutiwa mno mipango ya Waarabu hao, kubwa ni chuo cha soka ya vijana.
    Micho aliwaambia viongozi wa Yanga, kipindi hicho ikiongozwa na Francis Kifukwe, kwamba wanapokwenda nchi za watu kwenye mechi wasiende kushangaa maghorofa tu, wajifunze pia na mipango ya soka ya kisasa, ikiwemo hilo la soka ya vijana.
    Kwa mfano klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ina chuo chake cha soka kilichoanzishwa chini ya Roger Ouegnin na Jean-Marc Guillou mwaka 1993 katika Viwanja vya mazoezi vya ASEC.
    ASEC iliwekeza kwa watoto hao, ikianzia kuwapa elimu kwani walikuwa wakiingia darasani kufundishwa masomo ya Hesabu, Historia, Jiografia, Fizikia, Kifaransa, Kiingereza na Kispanyola. Wanafunzi waliishi kwenye mabweni (Yanga, Simba wana majengo wanaishi mbu tu), walikuwa wana ratiba ya kufany7a mazoezi mara mbili kwa siku na kucheza mechi kila siku ya Jumamosi sambamba na kupata huduma za Kiafaya.
    Nini matunda yake? Klabu hiyo imeweza kuuza yosso kibao Ulaya kuanzia wakiwemo Kolo Toure, Aruna Dindane, Salomon Kalou, Didier Zokora, Yaya Toure, Emmanuel Eboue na Gilles Yapi.
    ASEC pia imekuwa ikipeleka yosso wake wanaofaulu mafunzo chuoni hapo katika klabu za K.S.K. Beveren ya Ibelgiji, ambayo imekuwa ikivitambulisha vipaji vya chipukizi wa Ivory Coast na baadaye kununuliwa na klabu kubwa Ulaya.
    ASEC pia ilifunga ndoa klabu ya Charlton Athletic ya England, Mei Mosi mwaka 2006, inayomaanisha kwamba Charlton itakuwa inanufaika na chuo cha klabu hiyo.
    Ikiwa chini ya kocha aliyefanya makubwa nchini Angola, Dusan Kondic, Yanga ina nafasi kubwa ya kunufgaika na mpango huo.
    Kondic aliyeiongoza Primeiro de Agosto kutwaa ubingwa wa nchi hiyo misimu ya 1991 na 1992, pia amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Angola ilipokuwa ikiwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994, ikiundwa na nyota kama Ivo Traca.
    Kwa sababu hiyo, iwapo viongozi wa klabu hizo watakubali kufuata maelekezo ya Azimio la Bagamoyo, upo uwezekano wa kuvuna matunda yake.
    Lakini kama wataendelea kukaidi agizo hilo, basi chini ya viongozi wa aina hii, Simba na Yanga hazitafika popote. Hadi Jumapili ijayo. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UBABAISHAJI WA VIONGOZI SIMBA, YANGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top