SIMBA jana iliwabwaga wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), Prisons ya Mbeya mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba imepanda hadi nafasi ya pili, nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga baada ya kufikisha pointi 23, sawa na Kagera Sugar, lakini Wekundu hao wa Msimbazi, wanapanda kwa wastani wao mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Bao la kwanza la Simba lilipatikana katika dakika ya kwanza mfungaji akiwa ni Ramadhani Chombo 'Redondo', kabla ya Yona Ndabila kusawazisha katika dakika ya 27, wakati dakika ya 31 Mussa Hassan Mgosi alifunga kwa mkwaju wa penalti, uliotolewa na mwamuzi, Ahmed Kikumbo wa Dodoma baada ya Redondo kuangushwa eneo la hatari.
Emeh Izuchukwu, mshambuliaji wa Simba kutoka Nigeria, aliifungia timu yake bao la tatu dakika ya 60 akiunganisha kona ya Nassor Said ‘Cholo’ ambayo iliwachanganya mabeki na kipa wa Prisons kabla ya kumkuta mfungaji.
Baada ya mechi hiyo, Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema kwamba wachezaji wake walicheza vizuri ndio maana walishinda.
"Kuondoka kwa Henry Joseph kumeweka pengo, lakini naamini Aziz ameziba…," alisema Phiri.
Kwa upande wake, kocha wa Prisons, James Nestory, alisema licha ya wachezaji wake kucheza vizuri, lakini makosa madogo madogo waliyofanya Simba waliayatumia vizuri.
0 comments:
Post a Comment