Wababe wa kihistoria
Afrika Mashariki na Kati
na mahmoud zubeiry
RASMI mashindano ya soka Afrika Mashariki na Kati yalianza mwaka 1926, yakiwa yanashirikisha timu za taifa za nchi za ukanda huu. Mashindano hayo yalijulikana kwa jina la Kombe la Gossage.
Jumla ya mashindano 37 ya Kombe la Gossage yalifanyika tangu mwaka 1926 hadi 1966 kabla ya kubadilishwa na kuwa michuano ya Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki Kati.
Taratibu, CECAFA iliendelea kupanua wigo wa michuano yake, kwa lengo la kukuza soka ya eneo lake, na mwaka 1974 ilianza michuano ambayo ilitokea kuwa na msisimko mkubwa zaidi iliyojulikana: Klabu Bingwa ya Soka Afrika Mashariki na Kati.
Jumla ya mashindano 32 yamekwishafanyika hadi sasa tangu mwaka huo 1974, ingawa ni mwaka mmoja tu, 1990 yaliposhindwa kufanyika kutokana na kukosa mwenyeji.
Lakini miaka ya baadaye, michuano hiyo kidogo ilianza kupoteza msisimko kutokana na kukosa wadhamini, hata wa kutoa zawadi pekee, kabla ya mwaka 2002 kujitokeza Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame kujitiwisha mzigo huo.
Pamoja na kutoa za zawadi kwa washindi Rais Kagame amekuwa mstari wa mbele kwa nchi yake kuyapokea mashindano hayo kama nwenyeji.
Kwa sababu hiyo, tangu mwaka 2002, michuano hiyo imebadilika na kuwa Kagame Cup(Kombe la Kagame).
Mwaka huu, michuano hiyo ikiwa inafanyika Dar es Salaam, imepokea neema moja, baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Castle, kujitokeza kuidhamini.
Katika mashindano hayo, Simba SC ya Tanzania, inaongoza kutwaa Kombe hilo mara nyingi, ikiwa imeweza kufanya hivyo, mara sita, ikifuatiwa na AFC Leopards, zamani ikijulikana kama Abaluhya iliyoshinda taji hilo mara tano.
Tusker FC ya Kenya pia, zamani ikijulikana kama Kenya Breweries, inashika nafasi ya tatu kwa kutwaa taji hilo mara nne, wakati ndugu zao Gor Mahia, wamo kwenye orodha ya klabu zilizotwaa taji hilo mara tatu.
Ukiondoa Gor, klabu nyingine zilizotwaa taji hilo mara tatu ni pamoja na SC Villa ya Uganda, zamani ikijulikana kama Nakivubo Villa na Young Africans (Yanga) ya Tanzania.
APR FC ya Rwanda imetwaa taji hilo mara mbili sawa na Luo Union ya Kenya na El-Merreikh ya Sudan, wakati KCC, Polisi FC za Uganda na Rayon Sports ya Rwanda, zote zimetwaa taji hilo mara moja kila moja.
Kwa maana hiyo, Kenya inaongoza kutoa mabingwa wengi hadi hivi sasa ikiwa klabu zake zimetwaa taji hilo mara 14, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa klabu zake kutwaa taji hilo mara tisa.
Uganda imeweza kutoa mabingwa watano tu, wakati Rwanda imefanya hivyo mara tatu na Sudan mara mbili.
Lakini ukienda kwenye suala la klabu gani ni zaidi katika michuano hiyo, jibu ni Wekundu wa Msimbazi, Simba SC.
Simba imekuwa yenye bahati zaidi, michuano hiyo inapofanyika kwenye ardhi ya Tanzania, iwe Bara au visiwani, kwani mataji yake yote sita imeyavuna nyumbani, tofauti na watani wao wa jadi, Yanga waliotwaa mataji mawili mjini Kampala, Uganda na moja Zanzibar, ambalo ndilo lilikuwa la kwanza, mwaka 1975.
SIMBA WALIVYOTWAA UBINGWA 1974 DAR:
FILIMBI ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa ya Soka Afrika Mashariki na Kati, ilipulizwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Michuano hiyo ya kwanza ilifanyika kwa mtindo wa Ligi, ikishirikisha timu nne ambazo ni wenyeji Simba, Abaluhya FC ya Kenya, Navy ya Zanzibar na Simba FC ya Uganda.
Simba ya Uganda ilianza kwa kulazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na Navy FC kabla ya Wekundu wa Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kuwafunga Abaluhya FC bao 1-0.
Abaluhya FC ilihamishia hasira zake kwa Simba wa Uganda na kuibamiza mabao 3-1, wakati Wekundu wa Msimbazi waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwalaza jirani zao, Navy kwa bao 1-0.
Abaluhya walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Navy FC, hivyo kuiachia Simba ubingwa, kwani Wekundu wa Msimbazi walilazimisha sare ya bila kufungana na Mnyama mwenzao wa Uganda, Simba FC.
Kwa matokeo hayo, Simba ilimaliza michuano hiyo, ikiwa katika nafasi ya kwanza kwa kujikusanyia pointi tano kutokana na kushinda mechi mbili kutoka sare moja, enzi hizo mgawo wa pointi kwa mechi za kushinda, ikiwa ni pointi mbili.
Abaluhya ilimaliza ikiwa na pointi tatu kutokana na kushinda mechi moja, kufungwa moja na kutoka sare moja. Navy na Simba Uganda, kila moja ilimaliaza na pointi mbili kutokana na kutoka sare mbili kila moja.
Miongoni mwa wachezaji walioweka historia hiyo ya kuipa ubingwa wa kwanza Simba SC walikuwa ni Athumani Mambosasa, Shaaban Baraza, Mohamed Kajole,(marehemu), Hamisi Askari (marehemu), Omar Chogo (marehemu), Aloo Mwitu, Athumani Juma (marehemu), Haidari Abedi ‘Muchacho’, Willy Mwaijibwe (marehemu), Omar Gumbo, Khalid Abeid, Abdallah Kibadeni, Adam Sabu (marehemu) na Abbas Dilunga.
Hata hivyo, katika michuano iliyofanyika Zanzibar mwaka uliofuata, Simba licha ya kufanikiwa kuingia fainali, ilishindwa kutetea taji, baada ya kulala 2-0 mbele ya watani wao wa jadi, Yanga.
SIMBA YASHINDWA KUBAKISHA TAJI DAR 1977…
MWAKA 1977, michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, ilirejea Dar es Salaam na ilianza kutimua vumbi, Februari 4 kabla ya kufikia tamati siku 11 baadaye, yaani Februari 15.
Kundi la kwanza la michuano hiyo, lililokuwa na timu za mabingwa watetezi, Luo, KCC ya Uganda, Navy ya Zanzibar na Gor Mahia ya Kenya, lilitumia Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wakati kundi B lililoongozwa na wenyeji Simba SC, Horsed ya Somalia, Mufulira Wanderers ya Zambia na APR ya Rwanda.
Mabingwa watetezi, walinza kwa kuwafundisha adabu ndugu zao, Gor Mahia kwa kipigo cha mabao 4-2, wakati Navy iliitandika KCC 1-0, kabla na yenyewe kuchapwa 2-1 na Gor Mahia.
KCC ilionja ushindi wa kwanza dhidi ya Luo wa bao 1-0, kabla ya mabingwa hao watetezi kuhamishia hasira zao kwenye mechi yao iliyofuata dhidi ya Navy kwa kuwatandika mabao 3-1 na KCC iliichapa Gor 2-0 katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo.
Kwa matokeo hayo, Luo ilitinga nusu fainali kwa kutimiza pointi nne, ikifuatiwa na KCC iliyotimiza pointi kama hizo pia, lakini ikizidiwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika Kundi B, Simba SC ilianza kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana na Mufulira Wanderers, wakati Horsed iliitandika Rangers FC bao 1-0.
Mechi za mzunguko wa pili, Mufulira ililazimishwa sare ya 1-1 na Horsed, wakati Simba iliichapa Rangers FC mabao 2-0, kabla ya Mufulira kumalizia kwa sare na Rangers FC na Simba ikiilaza Horsed 1-0.
Kwa matokeo hayo, Simba iliongoza kundi B kwa kutimiza pointi tano, ikifuatiwa na Horsed iliyofikisha pointi tatu.
Wekundu wa Msimbazi wakiwa na matumaini ya kurudia kile walichokifanya mwaka 1974, walijikuta wakikwama katika nusu fainali baada ya bao pekee lililofungwa na Agondo Lukio, kudumu hadi mwishoni mwa mchezo.
Wasomali walioingia nusu fainali kwa staili ya kutoka sare tatu na kufungwa mechi moja, waliwastaajabisha mashabiki baada ya kuwafunga KCC na kukata tiketi ya kutinga Fainali.
Fainali kali na yenye kusisimua iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilishuhudia Wasomali wakitandaza kandanda safi uwanjani na kutishia uwezekano wa Luo kutetea ubingwa.
Horsed ilitangulia kufunga bao, lakini Agondo Lukio alifunga mabao yote mawili, yaliyoipa Luo ushindi wa 2-1, hivyo kufanikiwa kutetea ubingwa wao.
Kwa kufunga jumla ya mabao manne, Agonda Lukio alifanikiwa kujinyakulia kiatu cha dhahabu mwaka huo.
Baada ya hapo, mwaka 1978 Simba ilikwenda Kampala, Uganda kwenye michuano iliyofuata, ikiwa imejisahihisha kiasi cha kutosha.
Katika michuano hiyo, Simba ilitupwa kwenye kundi B sambamba na Luo Union ya Kenya na Hardware Stars ya Malawi, wakati Kundi A, liliongozwa na wenyeji KCC, Horsed na Navy ambayo tangu mwaka huo, ilianza kujulikana kwa jina la KMKM.
Ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 katika nusu fainali ya mwaka 1977, Simba iliyopangwa kufungua na Luo, iliingia kwa hasira kali na kulipa kisasi kwa ushindi wa aina hiyo hiyo, 1-0.
Luo Union nayo iliingia kwa hasira katika mchezo wake wa pili na kuilaza Hardware Stars mabao 2-1, kabla ya Simba kukamilisha mechi za kundi lake kwa ushindi wa 2-0, dhidi ya Wamalawi hao.
Kwa matokeo hayo, Simba ilitinga nusu fainali, baada ya kuongoza kundi B kwa kufikisha pointi nne, ikifuatiwa na Luo, iliyotimiza pointi mbili.
Katika nusu fainali, Simba iiliichapa Horsed 2-0, hivyo kukata tiketi ya kukutana kwenye fainali.
Katika fainali iliyochezeshwa na mwamuzi Nelson Chirwa kutoka Malawi, nyasi za Uwanja wa Nakivubo ziliwaka moto kweli kweli, wanaume wa Kampala na wanaume wa Dar es Salaam walionyeshana kazi na hadi dakika 120 zinamalizika, hakuna aliyefanikiwa kuliona lango la mwenzake.
Hatimaye mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti, na hapo ndipo SImba walipofeli, baada ya kuambulia kutumbukiza mikwaju miwili tu kimiani, kupitia kwa Abdallah 'King' Kibaden na Mohammed Bakari ‘Tall’, wakati Saad Ali shuti lake lilidakwa na kipa alipokwenda kujaribu kumtungua kipa mwenzake, alipiga juu ya lango.
KCC ilitumbukiza mikwaju yake kimiani kupitia kwa Moses Ssentamu, Philip Omondi na Tom Lwanga, wakati ‘bin Jabir’, Omar Mahadhi alipangua mikwaju ya Jamil Kasirye na Tim Ayieko.
Tangu hapo si Simba, Yanga wala klabu nyingine yoyote ya Tanzania, iliyoweza kufurukuta kwenye michuano hiyo, zaidi ya Wakenya na Waganda kupokezana taji.
SIMBA ILIVYOREJESHA KOMBE NYUMBANI 1991…
HATIMAYE baada ya miaka 15, Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, lilirejea Tanzania, baada ya SImba kulitwaa tena mwaka 1991 katika michuano iliyofanyika Dar es Salaam na Tanga.
Michuano hiyo ilishirikisha klabu za Gor Mahia ya Kenya, Limbe Leaf Wanderers ya Malawi, El-Mourada ya Sudan, SC Villa ya Uganda na wenyeji Simba SC na Coastal Union ya Tanga, iliyochezea mechi zake Tanga.
Coastal Union ilifanikiwa kuingia Nusu Fainali, lakini kitendo CECAFA kuitaka ikachezee mechi yake ya Nusu Fainali Dar es Salaam, kiliwakera Wagosi wa Kaya na kuamua kususia michuano hiyo katika hatua hiyo.
Kwa sababu hiyo, CECAFA iliipuuza Coastal na kuipa nafasi hiyo Limbe Leaf, iliyokuwa tayari imetolewa.
Simba nayo ilifuzu kuingia hatua hiyo, ambako iliitoa Gor Mahia, wakati SC Villa nayo ilivuka Nusu Fainali kwa kuifunga Limbe Leaf 3-1.
Katika michuano hiyo ambayo, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ aliibuka mfungaji bora kwa kufunga jumla ya mabao sita, Simba iliitandika 3-0 SC Villa kwenye fainali na kutwaa uibingwa huo.
Siku hiyo, kocha wa sasa wa Simba SC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alikuwa ana kazi moja tu ya kumdhibiti aliyekuwa mpachika mabao tegemeo wa Villa, Majjid Musisi asilete madhara.
Kipa wa Simba, Iddi Pazi ‘Father’, alidaka kwa kiwango kikubwa mno kwenye michuano hiyo, ambayo Simba iliwatoa machozi ya furaha mashabiki wake.
SIMBA WABABE TENA, WAINYUKA YANGA Z’BAR…
Baada ya kufanikiwa kurejesha taji nyumbani, Simba ilikwenda kutetea ubingwa wake visiwani Zanzibar mwaka 1992. haikwenda peke yake huko, iliongozana na watani wao wa jadi, Yanga ambao ndio walikuwa mabingwa wa Bara msimu wa 1991.
Katika michuano hiyo, iliyoshirikisha pia klabu za Bata Bullets ya Malawi, El Hilal ya Sudan, Small Simba na Jamhuri za Zanzibar, Rivatex Eldoret ya Kenya, Simba na Yanga walikutana tena kwenye fainali.
Mashabiki wa Yanga walijipa matumaini ya kutwaa taji hilo, wakiamini Zanzibar ni ardhi yenye baraka kwao. Mbwembwe za kila aina zilifanyika, enzi hizo klabu hiyo ikiwa chini ya mfadhili wake mkuu, Abbas Gulamali (sasa marehemu) aliyewahi pia kuwa Mbunge wa jimbo la Kilombero (CCM).
Hata hivyo, kwenye mchezo huo, Yanga ikinolewa Syllersaid Mziray, ilijikuta ikifungwa kwa mikwaju ya penalti, baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Mwaka 1993, Simba ilishindwa kutetea taji Kampala, Uganda na watani wao jadi, Yanga waliweza kuibuka mikono juu kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Hata hivyo, mwaka 1994, michuano iliyofanyika Sudan, Simba ilitolewa mapema kwenye kundi lake, A baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwa kuambulia pointi mbili, nyuma ya Express FC ya Uganda iliyoshika nafasi ya pili kwa pointi zake nne, wakati wenyeji El Merreikh waliongoza kundi hilo kwa pointi zao tano.
Yanga iliongoza kundi B, kwa kutimiza pointi nne, ikifuatiwa na El Hilal iliyofikisha pointi hizo pia, lakini ilizidiwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa na Watoto wa Jangwani, wakati Small Simba ya Zanzibar na Mebrat Hail (sasa EELPA) ya Ethiopia, ilishika mkia kwenye kundi hilo.
Katika nusu fainali, Yanga ilikutana na Express FC ambako baada ya sare ya bila kufungana, ilijikuta ikitolewa kwenye mikwaju ya penalti, baada ya kulala kwa penalti 5-4.
SIMBA WABAKISHA KOMBE DAR 1995…
Mwaka 1995, michuano hiyo ilirejea Tanzania na Simba ikafanikiwa kubakisha taji nyumbani.
Simba iliyoanza kwa sare ya 1-1 na Express FC ya Uganda, kabla ya kuzitandika Morris Supplies ya Somalia 3-1 na Adulis Djibouti 4-1, ilifanikiwa kuingia nusu fainali, ikitimiza pointi saba, mbele ya Express iliyofikisha pointi nne.
Katika kundi B, mambo hayakuwa mazuri kwa Yanga, kwani ilijikuta ikiambulia pointi mbili, baada ya sare za 1-1 na El Mourada ya Sudan na Malindi ya Zanzibar, mechi ambazo zilikuja wakati tayari Yanga imekwishafungwa 2-1 na Breweries (sasa Tusker) ya Kenya.
Yanga ilitolewa ikiwa na kikosi imara zaidi, kilichojumuisha damu changa, yaani wachezaji waliopandishwa kutoka kikosi cha pili, akiwemo Nonda Shabani ‘Papi’, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Galatasaray ya Uturuki.
Katika nusu fainali, Simba ilifanikiwa kuilaza El Mourada bao 1-0, hivyo kukutana na Express kwenye fainali, ambayo kwenye Nusu Fainali, iliitoa Breweries kwa kipigo cha mabao 2-0.
Dakika 120 za mchezo huo, zilimalizika kwa sare ya 1-1 na mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti, Wekundu wa Msimbazi walishinda kwa penalti 5-3.
Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 53, kupitia kwa beki wake mahiri enzi hizo, George Magere Masatu, lakini Hussein Amaan Marsha alijifunga dakika ya 51 na kuurefusha mchezo huo.
NI SIMBA TENA 1996…
Baada ya kutwaa taji hilo Dar es Salaam, michuano iliyofuata pia, Tanzania ilipewa uenyeji na watani wa jadi, Simba na Yanga wote walipata nafasi ya kwenda kufanya vitu vyao.
Simba ilipangwa kundi A, sambamba na klabu za Small SImba ya Zanzibar, Al HIlal ya Sudan na APR ya Rwanda, wakati Yanga ilikuwa kundi B sambamba na Gor Mahia ya Kenya, Express ya Uganda na Alba ya Somalia.
APR FC iliongoza Kundi A, kwa kutimiza pointi saba, ikifuatiwa na Simba iliyofikisha pointi sita, hivyo zote kutinga Nusu Fainali, zikiziacha Al Hilal ya Sudan iliyoambulia pointi tatu na Small Simba iliyomaliza ikiwa na pointi moja.
Kundi B nako, wageni wengine, Gor Mahia waliongoza wakitimiza pointi saba na kufuatiwa na Yanga, iliyofikisha pia pointi kama hizo, lakini ilizidiwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika nusu fainali, Simba iliiltoa Gor Mahia kwa kuichapa bao 1-0, wakati Yanga kwa mara nyingine, mikwaju ya penalti iliwaadhiri na kutolewa na APR kwa 4-2, kufuatia sare ya 2-2.
Ikijaribu kuwania nafasi ya tatu, Yanga ilifanya madudu zaidi, baada ya kutandikwa mabao 4-0 na Gor, wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kwa bao pekee la Bitta John dakika ya 115, iliweza kutetea ubingwa wake dhidi ya APR.
Tangu hapo, Simba SC iliyumba na kushindwa hata kuwika kwenye michuano ya nyumbani pekee, huku Yanga ikitawala.
Mwaka 1997, SImba haikwenda Zanzibar kutetea taji, zaidi ya Yanga pekee kwenda kupigana kiume hadi Nusu Fainali, ilikotolewa na AFC Leopards kwa mabao 2-1.
Mwaka 1998 visiwani Zanzibar, Yanga ilitolewa nishai na
Rayon Sport ya Rwanda iliyokuwa ikinolewa na Raoul Shungu, katika Nusu Fainali, baada ya kuchapwa mabao 3-1. Mwaka huo, wenyeji Mlandege walifika fainali na kufungwa 2-1 na Rayon, iliyoandika historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Rwanda kutwaa taji hilo.
Mwaka 1999, Yanga ilikwenda kutwaa taji hilo Uganda, wakiifunga SC Villa kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 4-1, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Mwaka 2000, Yanga iligoma kwenda kutetea taji Rwanda, baada ya kutopewa zawadi yake, dola 10,000 kutokana na kutwaa ubingwa wa mwaka 1999 nchini Uganda.
Mwaka 2001, katika michuano iliyofanyika Nairobi, Kenya Tanzania haikupeleka timu kutokana na kuwa kifungoni kwa adhabu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
SIMBA YARUDISHA KOMBE DAR 2002…
Hatimaye, mwaka 2002 visiwani Zanzibar, Simba ilifanya kweli tena katika michuano ya 29 ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Simba ilijinyakulia taji la sita kwenye michuano hiyo ya pili kufanyika chini ya udhamini wa Rais wa Rwanda, Meja Jenerali Paul Kagame, baada ya ile ya Nairobi, mwaka 2001.
Simba iliyotwaa taji hilo, baada ya kuifunga Prince Louis ya Burundi kwenye fainali bao 1-0, katika Nusu Fainali, iliwatoa wenyeji Mlandege kwa mabao 2-0.
Kwenye kundi lake, B Simba ilianza kwa sare ya bila kufungana na Elman ya Somalia, kabla ya kuifunga Prince Louis 2-1, Forodha ya Zanzibar 3-1 na Tusker ya Kenya 1-0, hivyo kuongoza kundi hilo kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Prince Louis iliyotimiza pointi saba.
Hata hivyo, katika michuano ya mwaka 2003, Simba ikiwa chini ya kocha yule yule aliyewapa taji Zanzibar, James Aggrey Siang’a, ilikwama mbele ya wenyeji SC Villa ya Uganda, waliokuwa wakinolewa na Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’, ambaye baadaye alikuja kuinoa na Yanga pia mwaka jana.
YASALIMU AMRI KWA FITINA ZA WAGANDA 2003…
Lakini kufungwa kwa Simba kwenye fainali, kulitawaliwa na mizengwe mingi, ikwemo kuahirishwa mechi ya mwisho bila sababu za msingi, tena taarifa zikitolewa dakika za lala salama, kuelekea kwenye usiku wa kuamkia siku ya mchezo huo.
Yanga pia ilishiriki michuano hiyo ya mwaka 2003, lakini ilitolewa mapema na kurejea Dar es Salaam mikono mitupu.
Taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo huo, ilidai eti sababu za msingi ni Februari 11 ilikuwa siku ya mapumziko kwa Waganda, hivyo fainali ikichezwa siku hiyo badala ya Februari 10, watu watamiminika kwa wingi kwenye Uwanja wa Namboole, unaojulikana pia kama Nelson Mandela.
Lakini ukweli ulikuwa ni kwamba Villa ilikuwa inakabiliwa na majeruhi, tena ambao ni wachezaji wake tegemeo, akiwamo aliyekuwa kipa wao enzi hizo Hannington Kalyesubula na washambuliaji Ekuchu Kasongo na Phillip Ssozi, ambao waliumia kwenye mechi ya nusu fainali.
Wachezaji wa Simba, waliokuwa wameumia kwenye mechi ya Robo fainali, dhidi ya Khartoum 3 ya Sudan, beki Victor Costa na mshambuliaji Emmanuel Gabriel, tayari walikuwa wamekwishapona.
Kweli, kwa njama hizo Villa ilifanikiwa wachezaji wake wote waliamka wakiwa fiti Februari 11 na kuingia uwanjani.
Lakini Simba ya wakati huo, ilikuwa ‘kamili’ ikiundwa na nyota kama Juma Kaseja, Said Sued, Ramadhan Wasso, Costa, Boniface Pawasa, Lubigisa Lubigisa, Selemani Matola, Steven Mapunda ‘Garrincha’, Edibily Lunyamila 48, Primus Kasonso, Emmanuel Gabriel, Madaraka Selemani 47, Athumani Machupa, Jumanne Tondola na Ulimboka Mwakigwe.
Pamoja na mwamuzi pia kuonekana kuwapendelea wenyeji, lakini mashabiki wa Villa walilazimika kusubiri hadi dakika ya 79, ili kushangilia bao pekee la mchezo huo lililowapa ubingwa, ambalo lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mkenya Vincent Tendwa.
Tendwa alifunga bao hilo, baada ya kupokea ‘pande’ safi kutoka kwa kiungo ambaye baadaye alihamia Simba, Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Tukio moja kubwa la kukumbuka baada ya mechi hiyo ni makocha wa Villa wakati huo, Milutin Sredojevic ‘Micho’ kutwangana na wa SImba wa enzi hizo, Siang’a.
Tangu hapo, Kombe la Kagame limekuwa likifanya ziara kati ya Rwanda na Uganda na sasa linashikiliwa na APR, waliokuja nalo Dar es Salaam.
MAKUCHA YA SIMBA YAPOTEZA MAKALI…
Mwaka 2005 katika michuano iliyofanyika Mwanza,
2005, Simba ilitolewa mapema kwenye Kundi lake A, baada ya kushika nafasi ya tatu, huku SC Villa iliyoongoza kundi hilo ikifuatiwa na Rayon zikitinga Nusu Fainali.
Mtibwa Sugar ndiyo timu ya Tanzania iliyofanya vizuri zaidi mwaka huo, baada ya kufika nusu fainali na kutolewa na SC Villa ya Uganda kwa kufungwa 1-0.
Katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu, Mtibwa ilifungwa kwa mikwaju ya penalti na Rayon, baada ya sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Mwaka 2006, katika michuano iliyofanyika Dar es Salaam, Simba ilitolewa kwenye Robo fainali na Moro United ya Morogoro kwa kufungwa 2-1, wakati Yanga nayo ilikwama kwenye hatua hiyo kwa kulala 1-0 mbele ya Polisi Uganda walioibuka mabingwa baadaye.
Polisi waliifunga Moro 2-1, mbele ya Rais Jakata Kikwete kwenye Uwanja wa Taifa wa zamani, Dar es Salaam.
Mwaka jana Yanga ilikwenda Rwanda kuwania taji, lakini ikarejea mikono mitupu baada ya kutolewa mapema tu kwenye kundi lake A, ikiambulia nafasi ya tatu, wenyeji APR waliibuka mabingwa baadaye wakiongoza kundi hilo, wakifuatiwa na URA. Pamoja na yote, ukisoma historia ya michuano hiyo, Simba ndio mabingwa wa kihistoria. Je, mwaka huu watarejesha makali yao? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA KAGAME:
1974 Simba SC (Tanzania)
1975 Yanga (Tanzania)
1976 Luo Union (Kenya)
1977 Luo Union (Kenya)
1978 KCC (Uganda)
1979 Abaluhya (AFC Leopards)
1980 Gor Mahia (Kenya)
1981 Gor Mahia (Kenya)
1982 AFC Leopards (Kenya)
1983 AFC Leopards (Kenya)
1984 AFC Leopards (Kenya)
1985 Gor Mahia (Kenya)
1986 El-Merreikh (Sudan)
1987 SC Villa (Uganda)
1988 Breweries (Kenya)
1989 Breweries(Kenya)
1990 Michuano haikufanyika
1991 Simba SC (Tanzania)
1992 Simba SC (Tanzania)
1993 Yanga (Tanzania)
1994 El-Merreikh (Sudan)
1995 Simba SC (Tanzania)
1996 Simba SC (Tanzania)
1997 AFC Leopards (Kenya)
1998 Rayon Sports (Rwanda)
1999 Yanga (Tanzania)
2000 Tusker FC (Kenya)
2001 Tusker FC (Kenya)
2002 Simba SC (Tanzania)
2003 SC Villa Uganda)
2004 APR FC (Rwanda)
2005 SC Villa (Uganda)
2006 Polisi (Uganda)
2007 APR FC (Rwanda)
2008 Tusker FC (Kenya)
0 comments:
Post a Comment