// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MAULID DILUNGA: Nyota wa kombaini ya Afrika 1973 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MAULID DILUNGA: Nyota wa kombaini ya Afrika 1973 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, January 26, 2009

    MAULID DILUNGA: Nyota wa kombaini ya Afrika 1973


    Dilunga mwenye suti nyeusi pichani kabla ya mechi ya ufunguzi Uwanja mpya, Taifa Stars The Cranes, mwaka 2007.

    Nilipata fursa ya kufanya mahojiano na Maulid Bakari Dilunga, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa Tanzania, aliyefariki dunia, Juni 10, mwaka 2008, nyumbani kwake Magomeni, wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Na hii ndio makala iliyotokana na mahojiano hayo, Mwenyezimungu amuweke pema peponi daima. Amin.

    AKIWA mwanafunzi wa mwaka wa mwisho kwenye Shule ya Sekondari Mzumbe ya Morogoro, alichukuliwa na klabu kongwe ya soka ya Tanzania, Yanga ya Dar es Salaam.
    Hiyo ilikuwa ni mwaka 1966. kutokana na uwezo wake wa kutandaza kabumbu ya uhakika, ilimchukua mwaka mmoja tu kuchaguliwa katika timu ua taifa ya Tanzania Taifa Stars.
    Huyo ni Maulid Bakari Dilunga, mmoja wa wanasoka bora kabisa kuwahi kutokea Tanzania.
    Wakati anaingia Yanga, Dilunga alikuwa pamoja na nyota wengine wa Morogoro, Mohamed Msomali na Abdulrahman Juma (sasa marehemu).
    Mshambuliaji huyu alikuwa na kipaji cha hali ya juu. Sasa hivi hakuna kama yeye. Alikuwa anacheza kwa kutumia akili, sambamba na kipaji alichojaaliwa na Mungu.
    Alikuwa na staili ya kufunga mabao kwa kuunanisha moja kwa moja wavuni. Alikuwa na uwezo wa kupiga chenga hata watu wane anasema kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Bara, Marijani Shaaban ‘Kabambe.’ “Ilikuwa ni vigumu kumpokonya mpira akiwa nao miguuni.”
    Akizungumza nyumbani wake Magomeni, wilayani Kilosa mkoani Morogoro hivi karibuni, Dilunga anasema siri ya mafanikio yake katika soka ni kuupenda mchezo wenyewe.
    “Soka iko ndani ya damu yangu. Tangu nina miaka mtiano, nilikuwa ninashangaza watu. Kwa hiyo, yaani sijui niseme nini. Any way, soka ni kipaji nilichojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” anasema Dilunga.
    Dilunga alifanya mengi enzi zake, ambayo mpaka leo yamezungumzwa kama vile alivyofanya mwaka 1973 katika michezo ya Afrika (All African Games), mjini Lagos, Nigeria.
    Katika michuano hiyo, Tanzania ilifanikiwa kufika nusu fainali iliyochezwa katika mtindo wa ligi. Katika mechi hizo, ilitoka sare mbili na kufungwa ya mwisho na Algeria.
    Kabla ya kufika nusu fainali hiyo, Tanzania ilizitambia timu mbalimbali, wakiwamo wenyeji Nigeria walioingia timu mbili A na B.
    “Tulitoka suluhu na Nigeria A, B tuliwagonga 2-1. Ghana na Togo, kila mmoja tulimchapa bao 1-0,” anasema Dilunga. “Mabao yote nilifunga mimi.”
    Dilunga anasema katika nusu fainali hizo kwenye Uwanja wa Surulere, Lagos, walitoka suluhu na Nigeria, kabla ya kutoak sae 1-1 na Misri.
    Anasema kwamba walishindwa kusonga mbele, baada ya kufungwa mabao 2-1 na Algeria.
    “Kwa hiyo, sisi na Misri tulitoka, Nigeria na Algeria wakacheza fainali,” anasema.
    Pamoja na Tanzania kutolea katika hatua ya nusu fainali, Dilunga anasema hawezi kuisahau michuano hiyo kutokana na kuchaguliwa katika kikosi cha kombaini ya Afrika, ambacho kilizunguka mataifa sita ya Amerika na Ulaya, kucheza mechi za kirafiki.
    Anayataja mataifa hayo kuwa ni Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru, Hungary na Bulgaria. Anasema kuwa katika ziara hiyo, walishinda mechi tatu, walitoka sare mbili na kufungwa moja.
    Mbali na Dilunga, pia alikuwapo Mtanzania mwingine, kipa wa zamani wa kimataifa, Omar Mahadhi, ambaye sasa ni marehemu.
    Hata hivyo, Dilunga anasema uteuzi wake, uliingiwa na utata, baada ya chama cha Soka Tanzania (FAT), kudhani kwamba mchezaji aliyeteuliwa timu hiyo ni Abdallah Kibadeni.
    “Walisema wanamtaka namba kumi. Stars enzi hizo namba kumi tulikuwa mimi na Kibadeni, kwa hiyo ikabidi sasa FAT iombe ufafanuzi kutoka CAF,” anasema. “Ndipo walipoambiwa tunamtaka Maulid Dilunga.”
    Anasema kwamba kilichowavutia CAF kumwingiza kwenye timu hiyo ni uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao, ikiwamo kuwalaza hoi wenyeji Nigeria B.
    Katika mechi hiyo, anasema kuwa aliingia dakika za lala salama, huku Stars ikiwa nyuma kwa bao 1-0, lakini alipachika mawili.
    Anasema kwamba katika kikosi cha kombaini ya Afrika, aliteuliwa kuwa nahodha, akisaidiwa na wachezaji wawili kutoka Misri na Algeria.
    Jambo jingine analojivunia Dilunga katika maisha yake ya soka, ni kufunga mabao manne, kati ya matano ambayo timu yake ya Yanga iliifunga Simba mwaka 1967 kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    “Mabao mawili nilifunga kwa penati, mawili kawaida,” anakumbuka Dilunga. “Moja lilifungwa na Saleh Zimbwe.
    Pia Dilunga alikuwamo katika kikosi cha Bara kilichotwaa Kombe la Challenge kwa mara ya kwanza mwaka 1974.
    Katika mechi ya fainali, Bara iliifunga Uganda kwa penati 5-4, yeye akiwa mmoja kati ya waliokwamisha mikwaju hiyo.
    Dilunga anasema kwamba, aliwahi kupata nafasi ya kucheza soka Ulaya mwaka 1970, wakati timu ya daraja la pili ya England, West Bromwich ilipozuru Tanania. Lakini anadai kwamba Mwenyekiti wa FAT enzi hizo, Said El Maamry alimzuia ili achezee timu ya Taifa.
    “Ilikuwa mwaka 1970, jamaa walikuja kama wageni wa Yanga. Tulicheza nao mpira, walinipenda sana na kutaka kunichukua,” anasema Dilunga.
    “El-Maamry akanizuia, alisema niisaidie timu ya taifa. Halafu na kipindi kile, mwamko ulikuwa mdogo.”
    Akizungumzia soka ya sasa Tanzania, Dilunga anasema imedoda mno kulingana na miaka ya nyuma.
    “Nashangaa magazeti yanaandika Tanzania haijawahi kuifunga Ghana, ni uongo,” anasema.
    “Enzi zetu sisi tumeshawafunga sana Ghana, mojawapo kwenye michezo ya Afrika kule Lagos 1973, tuliwafunga 1-0 na kuwatoa mashindanoni. Tena bao lenyewe nilifunga mimi mwenyewe.”
    Anasema sababu ya kudorora kwa soka ya Tanzania, ni kukosekana kwa makocha wenye ujuzi na kukosekana mipango madhubuti ya kuinua mchezo wenyewe, kama vile kuanzisha timu za watoto.
    Anawazungumzia wanasoka wa leo na kusema kwamba ni Edibily Lunyamila wa Yanga pekee, ambaye angalau anacheza soka ya kuvutia.
    Dilunga ametokea wapi hadi kufika kupeperusha bendera ya Tanzania katika soka ya Afrika?
    Alizaliwa Oktoba 9, 1949 huko Kisarawe, Pwani, alisoma shule ya Kati Kisarawe, kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Lyamungo, mkoani Kilimanjaro.
    “Lyamungo nilisoma darasa la tisa tu, kumi haid kumi na mbili niliwenda kumalizia Mzumbe Morogoro.” Anasema Dilunga.
    Wakati huo, tayari alikuwa ameshaiva kisoka na kuichezea KOmbaini ya Morogoro, tangu mwaka 1964, akiwa darasa la 11.
    Aliingia Yanga mwaka 1966, ambako aliichezea hadi mwaka 1974, alipohamia Simba, ambayo hata hivyo hakukaa muda mrefu.
    Alicheza Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, mjini Zanzibar.
    Katika fainali, walikutana na timu yake ya zamani na watani wa jadi, yanga kwenye Uwanja wa Amaan. Yanga ikiwa chini ya kocha Tambwe Leya, iliibugiza Simba mabao 2-1 na kuipokonya taji hilo.
    Nilipokuwa Yanga, niliifunga sana Simba. Lakini nilipokuwa Simba sikuifugna hata bao moja Yanga,” anasema Dilunga.
    “Siku hiyo tunafungwa na Yanga 2-1 Zanzibar, bao letu alifunga Kibadeni. Yale ya yanga, yalifungwa na marehemu Gibson Sembuli na Sunday “Computer’ Manara.”
    Hata hivyo, mgogoro ulioikumba Simba mwaka 1975 na ksuababisha timu hiyo kugawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu, ulimfanya Dilunga naye apoteze mwelekeo.
    “Mimi nilikuwa mmoja kati ya wachezaji waliokwenda Nyota Nyekundu,” anakumbuka mshambuliaji huyo aliyeichezea timu hiyo hadi mwaka 1978, alipostaafu soka moja kwa moja.
    “Mwaka wa kwanza nilikuwa kapteni, uliofuata nilikuwa kocha mchezaji hadi 1978 nilipostaafu.”
    Baada ya kuacha soka, Dilunga aliajiriwa na Kampuni ya Vifaa vya Ujenzi ya BHESCO, ambayo ilikuwa ya pili kwake. Mara baada ya kutoka shule mwaka 1966, aliajiriwa na Mamlaka ya Bandari.
    Alifanya kazi BHESCO hadi mwaka 1982. Hata hivyo wakati akifanya kazi BHESCO, alikuwa akiifundisha Pan Africans waliokuwa Yanga.
    Mwaka 1982 aliajiriwa na Kampuni ya Viatu (Bora), ambayo aliitmikia hadi mwaka 1995, alipohamia Kiwanda cha Mazulia, Kilosa, Morogoro.
    Aliajiriwa na Mazulia baada ya kauhitimu Stashahada ya Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Maendeleo ya Uongozi (IDM Mzumbe) mwaka 1994.
    Katika kiwanda hicho ambacho alikuwa Ofisa Utumishi, alifanya kazi hadi mwaka 1997, wakati kilipobinafsishwa na yeye kuangukia katika kilimo.
    Mbali na kufanya kazi Mazulia, pia alikuwa akiinoa timu ya soka ya kiwanda hicho, ambayo ilivunjwa mwaka 1997. Sasa Dilunga wa timu nyingine ya Kilosa, Bafana Bafana iliyopo Ligi Daraja la tatu.
    Dilunga ambaye alichezea Stars kwa miaka tisa, kuanzia 1967 hadi 1976 ni kocha aliyepata kozi fupi fupi hapa nchini, zikiwamo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la Dunia (FIFA).
    Mkongwe huyo ambaye mtoto wa baba yake mdogo, Abbas Dilunga naye alitamba Simba katika miaka ya 1970, anasema kwamba kozi hizo ni Preliminary mwaka 1982, Intermediate mwaka 1988 na Advanced alizosomea mara mbili 1983 na 1990.
    Dilunga ana watoto sita, wawili akiwa amezaa na Esther, ambao ni Mwahija aliyeolewa Tanga na Dilunga anayechezea timu ya Tazara ya Mbeya.
    Wengine amezaa na mke wake wa sasa, aitwaye Watende. Anawataja watoto hao kuwa ni Mzee, Bakari, Asha na Rehema.
    Nyota huyo anaishi bila ya wazazi wake, baba yake alifariki mwaka 1972 na mama yake mwaka juzi.
    Dilunga anazungumzia maisha yake kijijini, Kilosa na kusema kuwa ingawa yana tofauti kubwa na mjini, lakini amezoea na anaishi bila wasiwasi.
    Dilunga anasema kwamba licha ya kuwahi kuchezea Simba, lakini yeye ni mpenzi mkubwa wa Yanga. “Loh aisee, naipenda sana Yanga,” anakiri. Simba nilikwenda tu kwa ajili ya maslahi, lakini timu yangu ni Yanga.” Kwa kweli, Dilunga alikuwa wa pekee Tanzania. Je, atatokea mwingine kama yeye?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAULID DILUNGA: Nyota wa kombaini ya Afrika 1973 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top