// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); Kinonondi ijivunie warembo, bendi, lakini si soka… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE Kinonondi ijivunie warembo, bendi, lakini si soka… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Thursday, January 22, 2009

    Kinonondi ijivunie warembo, bendi, lakini si soka…


    Nancy Sumary, hiki ndio kitu ambacho Manispaa ya Kinondoni itajivunia zaidi, binti huyu alikuwa Miss Kinondoni mwaka 2005, akawa Miss Tanzania na Miss World Afrika mwaka huo huo. Kwenye soka klabu yao Villa Squad inachungulia kaburi.


    na mahmoud zubeiry
    MRATIBU wa timu ya Ilala, Said Tully hakuwa amekosea hata kidogo kusema kwamba mechi ya Robo Fainali kati yao na Pwani, kwao ndiyo ilikuwa fainali.
    Kwani walikutana na timu ngumu, pengine bora kuliko zote zilizoshiriki michuano hii na wakafanikiwa kushinda 2-0 ndani ya dakika 207.
    Mechi ya kwanza ilivunjika katika dakika ya 117, baada ya giza kuingia uwanjani na timu hizo zikiwa hazijafungana.
    Mchezo wa marudiano ulimalizika ndani ya dakika 90 kwa mabao ya Mohamed Kijuso na Athumani Machuppa kuipeleka Ilala nusu fainali, ambako ilikutana na Arusha na kuibwaga 2-0.
    Juzi kwenye Uwanja huo huo wa Taifa, Dar es Salaam, Ilala ilikutana na Kinondoni katika fainali ya kuwania Kombe la Taifa.
    Tofauti na mechi zilizopita za Ilala za Robo na Nusu Fainali, juzi Ilala walicheza mechi laini na kuibuka na ushindi mnoono wa mabao 5-0.
    Huo ulikuwa ni mchezo mwingine mwepesi mno kwa Ilala, baada ya ule wa kwanza dhidi ya Lindi, ambayo ilichezea mabao 10-1.
    Mafanikio ya Ilala katika michuano hii hakika yanatokana na mafanikio ya mkoa wenyewe kisoka, tayari upo katika kiwango cha juu ukiwa na wachezaji wa kutosha walioiva na kukomaa kisoka.
    Ingawa wengi walibeza kitendo cha Ilala kutumia wachezaji wa Simba na Yanga, lakini walikuwa wanauonea mkoa huo kwani ni halali yao kabisa kutumia wachezaji hao.
    Ilala ilifuata na kutekeleza kanuni katika uteuzi wa kikosi chake, ikitumia wachezaji wa klabu za eneo lake, ikiwatenga wachezaji ambao hawajacheza Ligi katika klabu za Ilala.
    Ilala haikuita mchezaji hata mmoja wa timu ya taifa, kwa sababu mapema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilionya, wachezaji wa Taifa Stars wasiguswe.
    Ilala ilifanya kama ilivyofanya Morogoro, iliunda kikosi chake kutokana na wachezaji wa timu za Polisi Morogoro, Moro United na Mtibwa Sugar, zote za Ligi Kuu.
    Halikadhalika kikosi cha Dodoma kilisheheni wachezaji wa Polisi Dodoma ya Ligi Kuu, kikosi cha Kagera, kilisheheni wachezaji wa Kagera Sugar ya Ligi Kuu kama ilivyokuwa kwa kikosi cha Mbeya, kilichokuwa na nyota wa Prisons ya Mbeya, iliyoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu.
    Kwa mantiki hiyo, dhana kwamba Ilala ilikosea kuita nyota wa Simba na Yanga, haina msingi wowote na haipingani na kanuni za Kombe la Taifa.
    Kwa upande mwingine, Ilala imethibitisha kwamba utawala wa klabu za Simba na Yanga katika soka ya Tanzania ni sahihi kabisa.
    Kinondoni haikuwa ‘saizi’ ya Ilala. Hata wangekutana kwenye mechi ya raundi ya kwanza, matokeo yasingekuwa tofauti na hayo.
    Kinondoni ni fukara aliyobobea kisoka kwa mikoa ya Dar es Salaam, kwani hata Temeke angalau imewahi kuwa na timu Ligi Kuu, ambazo ni Sigara na Trans Camp.
    Kinondoni ilifanikiwa kupata timu Ligi Kuu, Ambayo ni Twiga, lakini yenyewe ‘kwa njaa zake’ ikaamua kuiuza kwa Pan African.
    Hapo ndipo Kinondoni ilipojikuta inaiongezea nguvu Ilala, kwani kama kocha Jamhuri Kihwelo angepata muda wa kutosha wa kupitia pitia kumbukumbu za wachezaji waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu, angeweza kubeba baadhi ya nyota wa Pan kwenye timu yake.
    Pan japokuwa imeshuka kama Manyema FC, lakini ina wachezaji wazuri kama kipa Hajji Macharazi, viungo Samuel Ngassa, Salum Machaku na washambuliaji
    Rashid Roshwa na Suleiman Massawe.
    Kwa hivyo, Kinondoni haikuwa sawa ya Ilala kabisa na kipigo walichokipata ilikuwa sawa yao. Tena wana bahati watu kama Mussa Mgosi na Athumani Machuppa, siku hiyo hawakuwa sawasawa inavyotakiwa, vinginevyo wangekumbana na adhabu kama ya Lindi.
    Kama Temeke wasingefanya makosa ya kitoto, kutumia mchezaji ambaye hakucheza Ligi kwenye mkoa wao, bila shaka wangefika mbali na wangeweza kutoa upinzani wa kweli kwa Ilala.
    Temeke ingawa haina timu Ligi Kuu, lakini ina mipango ya kweli ya kutaka kuwa na timu Ligi Kuu na timu zake zinaonyesha ushindani wa kweli kwenye kuwania nafasi hiyo.
    Mbagala Market mwaka jana ilizidiwa kete kidogo na Coastal Union ya Tanga katika kuwania kupanda Ligi Kuu na sasa ipo tena kwenye kinyang’anyiro cha kuhakikisha inarejea Ligi Kuu.
    ‘Mabwana wakubwa’ waliounda Kamati ya Ushindi ya Kinondoni, akina Athumani Tippo, Dk. Maneno Tamba na wengine wote, wanapaswa kujua kwamba, wanatakiwa kwanza kuimarisha klabu za mkoa wao, ili kupata wachezaji bora.
    Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Fabian Massawe, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Kinondoni aliyehamishiwa Mwanza, Jamal Rwambow, wote hao ni wapenda michezo mashuhuri.
    Lakini Chama cha Soka Kinondoni (KIFA) kiliwashirikisha vipi watu hawa kuhakikisha mkoa wao unakuwa na timu za ushindani, ikibidi zicheze Ligi Kuu?
    Kwanza ilifikia hatua gani hata Twiga SC ikauzwa kwa Pan? Hilo ni swali ambao wapenzi wa soka Kinondoni wanapaswa kujiuliza na kung’amua mapema mno wapi walipojikwaa ni si walipoangukia.
    Kinondoni imekuwa ikitoa wachezaji wengi kwenda timu za mikoa mingine, kote nchini ikiwemo hiyo Ilala, lakini kwa nini yenyewe inashindwa kujijenga katika kiwango cha juu ili inufaike na nyota wake?
    Naam, wakati umefika sasa wadau wa soka Kinondoni waamue kujitolea kuitumikia soka na si kutafuta sifa zisizo na mpango.
    Waziimarishe klabu za mkoa wao, ziweze kushindana na kupanda Ligi Kuu.
    Kinondoni wajiulize, Ilala imekwishapeleka timu ngapi ligi kuu, wakati wao wanasuasua tu.
    Tangu mwaka 2000, imeshuhudiwa Pentagon, Vijana, Ashanti, na Manyema, ‘vyote ni vitimu vidogodogo’ vya Ilala vikicheza Ligi Kuu, vipi Kagera Rangers, Friends Rangers, Linea Messina, Sifa United, Villa Squad, Abajalo, Sinza Stars na Nondo?
    Hapo ndipo KIFA wajue kwamba wao wanacheza tu na hadi kufika fainali ya Kombe la Taifa, Mungu aliwapenda sana.
    Bila ya kuweka mikakati thabiti za kuzisaidia klabu za Kinondoni kupanda Ligi Kuu, basi wakazi wa Kinondoni watabakia kujivunia mataji ya ulimbwende ya Miss Tanzania, ambayo kila kukicha warembo wa mkoa huo wanapokezana.
    Zaidi ya hapo watajivunia bendi zao zinazotikisa jiji, FM Academia, Akudo Impact, Twanga Pepeta na Diamond Musica, lakini kwenye soka, Ilala ndiyo baba lao.
    (Makala hii iliandikwa baada ya michuano ya Kombe la Taifa mwaka jana, Ilala ikitwaa ubingwa)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: Kinonondi ijivunie warembo, bendi, lakini si soka… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top