“NILIPOITWA kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa, kocha aliniambia nijitahidi kupata timu kubwa ambayo nitacheza ili kujiongezea uzoefu utakaonisaiodia kupata nafasi kikosi cha kwanza Stars”
Taratibu alianza kuonekana katika benchi la timu ya taifa, wakati huo alikuwa akicheza soka Ashanti United ya Dar es Salaam iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya Tanzania (sasa inashiriki Ligi daraja la kwanza).
Ukimuangalia kwa mbali huwezi kufikiri kwamba an auwezo wa kufanya vitu adimu Uwanjani, ni kijana mfupi mwenye umbo la kiuanamichezo anayeweza kupiga miguu yote miwili lakini ule wa kushoto una nguvu zaidi kuliko wa kulia.
Anacheza namba tatu katika klabu yake ya Simba na timu ya taifa, kutokana na juhudi zake binafsi, ameweza kujitengenezea mazingira ya kuwamo katika kikosi cha kwanza katika timu zote mbili.
Anaitwa Juma Jabu Hamis kijana wa miaka 21 ambaye amezaliwa akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto watatu ya Mzee Hamis Jabu na mama Halima Jabu, kaka yake anaitwa Shaban na mdogo wake ni Nuhu.
“Nilijikuta nikipenda mpira hasa kutokana na kipaji nilichokuwa nacho, pia mtaani kwetu kitu kilichokuwa kikipendwa na vijana ilikuwa ni mpira wa miguu, hii ndiyo siri yangu ya kujiunga na soka.
Mwanzo nilikuwa nacheza kama burudani kwangu, lakini jinsi siku zilivyokuwa zinaenda ndivyo nilivyoanza kuwaza kucheza hatua fulani, wazazi wangu walitaka nisome zaidi,” anasema Jabu.
Anasema baba yake aliwahi kucheza soka katika klabu ya Reli ya Morogoro na Yanga B katika miaka ya 1980.
Alisoma shule ya msingi Karume ya Magomeni, Dar es Salaam kuanzi mwaka 1995 hadi 2001, kisha akajiunga Makongo sekondari mwaka 2002 hadi 2005. Alijiunga Makongo Sekondari akiwa kama mwanafunzi wa kawaida, kwani baba yake hakutaka ashiriki katika michezo badala ya masomo.
Mwaka 2006 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (Dar es Salaam Institute of Technology- DIT) kuchukua mafunzo ya usanifu na uchoraji (Graphics and Drawing) na kutunukiwa cheti. “Mpira umenifanya kuweka vyeti vyangu kabatini kwa muda ili niweze kutengeneza maisha yangu kupita huko, lakini baadae nitarudi katika taaluma niliyosomea na kufanya kazi yangu, ” anasema Jabu.
Ukimuuliza alianza mawaka gani kutandaza soka ya uhakika, atakwambia mwaka 1993 katika mitaa ya Magomeni Mwembechai katika timu ya Kagera Rangers akiwa na wachezaji kadhaa akiwemo Good Wambasa.
Alicheza katika timu hiyo kwa kipindi kirefu, kwani alipokuwa akitoka shule Makongo alikuwa anashiriki mazoezi ya timu hiyo, pia alipata bahati ya kuchaguliwa kuunda kikosi cha timu ya shule ya Makongo mwaka 2002.
Wakati anaingia shule alichukuliwa kama mwanafunzi wa kawaida, lakini baadaye aliyekuwa Mkuu wa Shule, Kanali Idd Kipingu alimpendekeza kuwa mwanafunzi mwanamichezo, hali iliyomfanya kusoma kwa punguzo la karo.
Mwaka 2004/5 alicheza katika timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa ikifundishwa na Abdallah Kibaden na Sylevester Marsh, timu hii ilikuwa ikishiriki michuano ya awali ya kombe la mataifa ya Afrika ya vijana. Alikuwa pamoja na wachezaji kama Nurdin Bakari, Athuman Idd ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Amir Maftah na Omari Matuta.
Baada ya kufanya vizuri katika timu hiyo, Jabu alisajiliwa na Kagera Sugar na kushiriki Ligi Kuu ya Tanzania mwaka 2005, kabla ya kuachana na soka mwaka uliofuata na kujiunga na DIT, lakini alirudi tena uwanjani mwaka 2007 na kujiunga na Ashanti United, huko alikutana na wachezaji kama Adam Kingwande, Jabir Idrissa, Juma Nyosso, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Maneno Uvuruge.
“Nakumbuka baada ya kufanya vizuri na Ashanti niliweza kusajiliwa na Simba baadaya msimu kumalizika, nilifurahi kutimiza ndoto yangu kwani kucheza katika timu kubwa kama hii ni ndoto ya kila mchezaji hapa nchini.
Nakubali ushindani ni mkubwa hapa (Simba), lakini kama inavyoona najitaidi kadiri ya uwezo wangu kuweza kuwamo katika kikosi cha kwanza,” anasema Jabu anayevutiwa na soka ya mchezaji mwenzake wa Simba na Ashanti zamani, Redondo.
Kwa kufuata ushauri wa kocha wa timu ya taifa, Marcio Maximo, Jabu ameweza kujiunga na Simba na kucheza katika timu hiyo sambamba na ile ya taifa kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuwa na namba ya kudumu katika vikosi hivyo.
Ufundi wa Jabu anayeweza pia kucheza namba sita, ulionekana katika mchezo dhidi ya Cape Verde pale alipoweza kuipangua ngome ya timu hiyo na kumpata pasi nzuri Mrisho Ngassa.
0 comments:
Post a Comment