MABINGWA wa Tanzania, Yanga wameanza vibaya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-0 nyumbani na Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo wa Kundi A Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao yaliyoizamisha Yanga leo yamefungwa na washambuliaji Adama Coulibaly wa Mali dakika ya 63 akimalizia pasi ya beki Altayeb Abdelrazig na Yasir Mozamil dakika ya 90 akimalizia pasi ya kiungo Abdel Raouf Yagoub.
Yanga leo iliongozwa na kocha mpya, Mjerumani mwenye asili ya Bosnia and Herzegovina, Sead Ramovic aliyechukua nafasi ya Muargentna Miguel Angel Gamondi aliyefukuzwa wiki iliyopita.
Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo Yanga kufungwa – pamoja na zile mbili za Ligi Kuu walizochapwa 1-0 na Azam FC na 3-1 na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam zilizomfukuzisha Gamondi.
Mechi nyingine ya Kundi A leo, wenyeji TP Mazembe wameambulia suluhu mbele ya MC Alger Uwanja wa TP Mazembe Jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Yanga watakuwa na mchezo mmoja wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC Jumamosi Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi kabla ya kusafiri kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa Kundi Ligi ya Mabingwa dhidi ya wenyeji, MC Alger Desemba 7 kuanzia Saa 4:00 usiku Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers.
0 comments:
Post a Comment