SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeongeza zawadi za ushiriki wa michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake barani kwa asilimia 52 na sasa litatumia kiasi cha dola za Kimarekani 2,350,000 jumla kwa sababu hiyo.
Taarifa ya CAF imesema kwamba kwa kufuzu tu kushiriki Fainali za Ligi ya Mabingwa Wanawake Afrika ambayo mwaka huu inafanyika nchini Morocco kuanzia Jumamosi ya Novemba 9 hadi 23, kila klabu kati ya zote nane itapata kiasi cha dola 150,000.
Ligi ya Mabingwa wa CAF ya Wanawake ni shindano jipya ambalo lilianzishwa chini ya uongozi mpya wa CAF wa Rais Dk Patrice Motsepe kuanzia mwaka 2021.
Zawadi ya bingwa msimu huu imeongezeka kutoka dola 400,000 hadi 600,000, wakati mshindi wa pili sasa atapata dola 400,000 badala ya 250,000 za awali.
Timu itakayomaliza nafasi ya tatu itapata dola 350,000, ya nne dola 300,000 wakati mshindi wa tatu wa Kundi atapata dola 200,000 na wa nne ni dola150,000.
CAF imejitolea kuendeleza na kukuza Soka ya Wanawake barani Afrika na lengo la Rais Motsepe ni kuwekeza katika Akademia za Vijana kwa wavulana na wasichana na kuendelea kuongeza fedha za zawadi za Mashindano yake yote ili kuyaongezea ushindani na mvuto wa kimataifa.
Timu zilizofuzu kushiriki michuano hiyo msimu huu ni pamoja na bingwa mtetezi, Mamelodi Sundowns, Chuo Kikuu cha Western Cape za Afrika Kusini, wenyeji FAR Rabat ya Morocco, Aigles de la Medina ya Senegal, EDO Queens ya Nigeria, FC Masar ya Misri, CBE FC ya Ethiopia na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
ZAWADI ZA LIGI YA MABINGWA WANAWAKE 2024:
Bingwa: USD 600,000Mshindi wa pili: USD 400,000
Nafasi ya 3: USD 350,000
Nafasi ya 4: USD 300,000
Nafasi ya 3 ya Kundi: USD 200,000 kila moja
Nafasi ya 4 ya Kundi: USD 150,000 kila moja
0 comments:
Post a Comment