Yussuf Bakhresa |
Na Mahmoud Zubeiry
WAKALA wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), Yussuf Said Salim Bakhresa yupo, Makka, Saudi Arabia kwa
ajili ya kufanya ibada ya Hijja kesho.
Yussuf ambaye ni mtoto wa bilionea, Said Salim Bakhresa,
mmiliki wa Azam FC, moja ya timu tishio katika Ligi Kuu nchini, anakuwa
miongoni mwa vijana wachache wa Kitanzania waliothubutu kutekeleza nguzo hiyo
ya tano ya Uislamu katika umri wa ujana.
Alhaj huyo mtarajiwa anakuwa kiongozi wa pili kijana katika
msafara wa Watanzania waliokwenda mwaka huu Hijja, baada ya Mwenyekiti wa
Yanga, Yussuf Mehboob Manji.
Yussuf Bakhresa pamoja na kuwa mtu muhimu katika ustawi wa
Azam, lakini pia amekuwa mfano wa mawakala wa wachezaji hapa Tanzania
waliofanya juhudi za makusudi kujaribu kuwatafutia timu Ulaya wachezaji nchini.
Amewahi kumpeleka Mrisho Ngassa katika klabu ya West Ham
United ya England ambako pamoja na kufuzu majaribio, akarudishwa Afrika
‘kuongeza lishe’. Amewahi kumpeleka John Bocco ‘Adebayor’ Israel ambako pia
alikubalika mno.
Yussuf pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bakhresa Food
Products Limited ingawa pia ni Mkurugenzi wa makampuni mengine yote ya Bakhresa,
chini ya Mwenyekiti, baba yao, Said Salim Awadh Bakhresa.
Wakurugenzi wengine wa Bakhresa Group Of Companies ni
Mohamed, Abubakar na Omar. Mohamed ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bakhresa Grain
Milling (Uganda) na Mkurugenzi Mkuu wa Said Salim Bakhresa & Company
Limited, wakati Omar ni Mkurugenzi Mtendaji Said Salim Bakhresa & Co Ltd na
Abubakar Mkurugenzi Mkuu wa Bakhresa
Grain Milling (Malawi) na Bakhresa Grain Milling (Msumbiji) Limitad.
Lakini pia Abubakar ni Mkurugenzi Mtendaji wa Said Salim
Bakhresa & Co. Ltd na wote ni Wakurugenzi wa bodi ya Azam FC chini ya
Mwenyekiti, mzee Said Salim Awadh Bakhresa.